KILIMANJARO-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuthibitisha kuwa yeye ni kiongozi madhubuti anayeweka maslahi ya Tanzania mbele.
Akizungumza kwenye hafla ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi, hafla ambayo pia iliadhimisha miaka 60 ya jeshi hilo, Rais Dkt.Samia amewapongeza askari polisi kwa kazi yao kubwa ya kulinda amani na utulivu wa taifa letu.
Rais amethibitisha kuwa, ataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Katika hotuba hiyo ya kihistoria, Rais Samia ameweka wazi kuwa Tanzania ni nchi inayojitegemea na yenye hadhi, na hivyo haiwezi kuamriwa na watu wa nje kuhusu jinsi ya kuendesha masuala yake ya ndani.
Pia,amekemea vikali kauli za kibaguzi zilizotolewa na baadhi ya balozi za kigeni baada ya kifo cha mwanachama wa Chadema,Ali Kibao.
Amefafanua kuwa, kauli hizo hazikutolewa kwa ridhaa ya serikali za balozi hizo, na akasisitiza kuwa balozi hizo zinapaswa kuheshimu mamlaka ya Tanzania kama vile balozi zetu zinavyoheshimu mamlaka za nchi nyingine na Tanzania haitaruhusu kamwe mataifa ya nje kutuamulia.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amefichua njama zinazofanywa na chama kimoja cha upinzani ambacho kilifanya mkutano huko Arusha tarehe 11 Septemba, ambapo ajenda kuu ilikuwa ni jinsi ya kutumia maandamano na vurugu ili kuvuruga serikali kwa matumaini ya kuipindua.
Hili ni jambo hatari na linaweza kuhatarisha usalama wa nchi yetu, jambo ambalo Rais alilieleza kwa uwazi kabisa.
Wananchi wanapaswa kuwa macho na kuepuka kujiingiza kwenye njama hizi za kipumbavu zinazoweza kuleta machafuko.
Rais Samia pia alitoa wito kwa vyama vya siasa nchini kuheshimu falsafa yake ya 4R’s (Maridhiano, Uvumilivu, Haki na Uwajibikaji) na kutochukulia kimzaha uhuru wa kisiasa wanaoufurahia sasa.
Aliwakumbusha kuwa, uhuru huu wa kisiasa umepatikana kwa jitihada kubwa, na hivyo ni muhimu kuutumia kwa busara, si kwa kuchochea vurugu na machafuko.
Kwa ujumla, hotuba ya Rais Samia imeendelea kudhihirisha uimara wa uongozi wake na dhamira yake ya kulinda taifa dhidi ya vitisho vyovyote vya ndani na nje.