NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga kuhakikisha maji yanapatikana ndani ya miezi mitatu.
Ni katika Mradi wa Maji wa Mtyangimbole uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Mradi huo ambao unagharimu shilingi bilioni 5.5 unatarajiwa kuvinufaisha vijiji vya Mtyangimbole, Gumbilo, Luhimba na Likalangilo.
Rais Dkt.Samia ametoa agizo hilo leo Septemba 24,2024 wakati akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo kwa niaba ya miradi 30 mkoani Ruvuma.
SOMA:Rais Dkt.Samia aweka jiwe la msingi mradi wa maji Mtyangimbole
"Nimeona mradi mzuri, maendeleo ni mazuri, ninawashukuruni sana Wizara ya Maji, Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa maji asanteni sana. Wanafanya kazi nzuri ambayo Serikali tumewatuma kufanya.
"Kwa hiyo ndugu zangu nimeona mradi, nimeona maendeleo, nimemwambia Waziri na Katibu Mkuu wake ambao ni wachapa kazi wazuri sana na watendaji wao ninawapa miezi mitatu tu.
"Siku sitini za kazi, mwezi mmoja kufanya yale ambayo mmechelewa kukamilisha maji yatoke kwa wananchi hawa.
"Kwa sababu leo tumekuja kuweka jiwe la msingi, tayari tumeshajenga matumaini kwao. Kwa hiyo baada ya miezi mitatu. Mwezi wa 12 Krismasi ikiingia maji yawe mwa...mwa..mwa ndani ya eneo hili,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.
Rais Dkt.Samia ameweka jiwe la msingi mradi huo wa tenki la maji Mtyangimbole ambao una uwezo wa kupokea lita milioni 1.9 na utahudumia wananchi zaidi 14,000 utakapokamilika.