Rais Dkt.Samia avutiwa na ubunifu wa Manispaa ya Songea ujenzi wa Chief Zulu Academy

RUVUMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kutenga fedha za mapato ya ndani zaidi ya shilingi milioni 600 na kujenga Shule ya Msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Chief Zulu (Chief Zulu Academy).
Mhe. Rais ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wazazi na wanafunzi baada ya kuzindua shule hiyo leo Septemba 24, 2024 Manispaa ya Songea.
“Ninawapongeza sana Manispaa ya Songea kwa kutenga fedha zaidi ya shilingi milioni 600 kutoka kwenye mapato yenu ya ndani na kuamua kujenga shule hii muhimu kwa taaluma ya watoto wa Mkoa wa Ruvuma.

"Nimefarijika kuona mmejenga kuanzia madarasa ya awali ambayo yanawasaidia watoto kwenye malezi na makuzi bora kabla hawajaanza darasa la kwanza,”amesema.

Aidha,amewataka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kutafuta walimu wabobevu wa kufundisha Lugha ya Kingereza ili watoto hao waijue lugha hiyo kwa ufasaha.
“Shule kama hizi zinazofundisha Kiingereza mnatakiwa kuweka walimu wanaoijua lugha hii vizuri ili kuwanoa watoto hawa kuwa mahiri kwenye lugha ya Kiingereza na sio Kiingereza cha kubabaisha,”amesema.

Aidha,Mhe. Rais amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha Sera ya Elimu ili kuendana na mabadiliko ya Dunia kwa sasa.

“Mnavyoendelea kuongeza shule za michepuo ya Kiingereza msisahau lugha yetu ya Kiswahili,lakini pia mkaangalia lugha nyingine tunayoweza kuwafundisha watoto wetu ambayo ni fursa huko Duniani kama Kichina, Kifaransa.
"Katika hili mnaweza kugawa mikoa kwa kanda,hivyo mikoa kadhaa ikawa na shule za kufundisha Kiingereza na lugha nyingine muhimu ya Kimataifa na shule za mikoa mingine nazo zikafundisha Kiingereza na somo lingine ili tuweze kuwa na wataalam wengi wa lugha wanaoweza kupata soko kimataifa,”amesema.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, hadi sasa nchini shule hizo za mchepuo wa Kiingereza ziko 68 ambazo zinafundisha lugha ya Kiingereza.
Shule ya Chifu Zulu ina wanafunzi wa awali na nsingi 491 na wanafundishwa masomo yote kwa lugha ya Kiingereza isipokuwa kwa somo la Kiswahili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news