Rais Dkt.Samia awaagiza wadau kuufanya Utamaduni kuwa biashara

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameziagiza wizara zinazohusika na masuala ya utamaduni na utalii kushirikiana na wadau wengine ili kuufanya utamaduni kuwa biashara.
Lengo ni kuhakikisha Watanzania wananufaika kupitia kazi zao za utamaduni, sanaa na ubunifu hapa nchini.

Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Septemba 23,2024 wakati akifunga Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa lililofanyika katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea Mkoa wa Ruvuma.
"Niwape moyo na niwatie ari Watanzania wenzangu ikiwemo wadau wa utalii kuona namna ya kuufanya utamaduni wetu kuwa biashara ili utuletee manufaa ya kiuchumi.

"Nataka niseme wakati ninazunguka kwenye mabanda ya maonesho nilipita katika banda la BASATA, nilifurahishwa sana kwa kweli kuona mabadiliko ya Sera ambayo BASATA inayafanya.
"Wanabadilika na kuufanya utamaduni, sanaa na ubunifu sasa kuwa ni ajira, kuwa ni biashara na kuwa ni uchumi.Sasa huu ndiyo mwendo wa kwenda nao BASATA, muendelee na msukumo huo."

Vilevile, Rais Dkt.Samia ameagiza matamasha yajayo yaboreshwe huku ushiriki wa sekta binafsi ukiongezeka zaidi.

"Tamasha kama hili likitangazwa linaweza kuwa jambo kubwa sana na mikoa itakuwa inaligombania kuwa wenyeji kwa sababu ni fursa nzuri ya kiuchumi, kuna watu ambao wametangulia kuja kwenye tamasha hili, baadhi yao kutoka Zanzibar wanasema Mama, Songea kumefurika hakuna pa kukaa."
Rais Dkt.Samia amesema hiyo ni fursa kubwa ambayo inakuja na tamasha hilo huku akiwataka Songea kujiandaa katika matamasha yanayokuja kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kuwekeza katika huduma za malazi na chakula.

Awali, Rais Dkt.Samia alitembelea Makumbusho ya Vita vya Majimaji iliyopo Mjini Songea mkoani Ruvuma kwa lengo la kutoa heshima ya Kumbukizi ya Mashujaa wa Vita ya Maji Maji vilivyopiganwa takribani miaka 119 iliyopita.
Rais Dkt.Samia akiwa katika makumbusho hiyo iliyobeba historia ya kipekee duniani alipokelewa na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wakiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana,

Katibu Mkuu,Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, uongozi wa Mkoa wa Ruvuma , Chifu wa Wangoni Zulu Gama 1, Wazee wa Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma na viongozi wa dini.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt.Samia alitembelea Ukumbi wa Historia ya Vita ya Majimaji, Onesho la Nyumba ya Inkosi (Chifu) wa Kabila la Wangoni.

Sambamba na kuweka shada la maua katika Kaburi la Halaiki la Mashujaa wa Vita ya Majimaji na Kaburi la Chifu Msaidizi (Nduna Songea Luwafu Mbano mjini Songea.
Pia,Rais Dkt.Samia ameweka silaha za jadi katika Mnara wa Kumbukumbu ya Mashujaa wa Vita ya Kagera.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news