Rais Dkt.Samia azindua Kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi wake)

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema mafanikio ya uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, yalichangiwa na uaminifu kwa mamlaka yake ya uteuzi, mapenzi yake kwa wananchi, uadilifu na uchapakazi.
Rais Dkt Samia amesema hayo kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu kuhusu Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Rais Dkt. Samia amesema Hayati Sokoine alitekeleza wajibu wake kikamilifu kama msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali katika kipindi kigumu na kusimama imara katika kipindi ambacho nchi ilikumbwa na changamoto za kiuchumi, uhaba wa chakula, miundombinu duni na changamoto katika sekta za viwanda na afya.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema maisha ya Hayati Sokoine yalikuwa na mafunzo mengi na uongozi wake uliacha alama katika kila jukumu alilokasimiwa.

Akizungumzia alama aliyoacha kwenye sekta ya Kilimo, Rais Dkt. Samia amesema Sokoine alisisitiza kilimo cha kisasa na chenye tija ili kukuza uchumi wa wananchi wengi vijijini. Katika kuenzi maono ya Hayati Sokoine katika sekta ya kilimo, Rais Dkt. Samia amesema Serikali za Awamu zote zimetoa kipaumbele kuendeleza sekta hiyo ikiwemo kwa kuongeza bajeti ya kilimo, ambayo imewezesha mageuzi makubwa katika sekta hiyo.

Jitihada hizi zilizoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita, zimewezesha Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128.

Rais Dkt. Samia ameahidi kuendelea kufanya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na kuongeza tija kwenye uzalishaji, kwa lengo la kufungamanisha kilimo na sekta ya viwanda kwa kuongeza thamani ya mazao.

Rais Dkt. Samia pia amesema alama nyingine iliyoachwa na Hayati Sokoine ni mchango wake katika ujenzi wa reli ya TAZARA iliyokuwa na mchango mkubwa katika vita vya ukombozi Kusini mwa Afrika, na ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuifufua kwa azma ya kutekeleza Dira ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063) na kurahisisha biashara baina ya nchi za Afrika.

Aidha, Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa viongozi na vijana kuhakikisha wanasoma kwa mazingatio kitabu kuhusu Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine kwa ajili ya kunufaka na mafunzo ya kiuongozi na historia ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news