Rais Dkt.Samia hayupo tayari kuona Sekta ya Kilimo inatetereka-Waziri Bashe

SHINYANGA-Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussin Bashe (Mb) amesema,Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hana deni kwa watanzania katika Sekta ya Kilimo,hivyo watendaji wa wizara wana wajibu wa kuhakikisha yote yanayofanywa na Serikali yanatekelezeka.
Amesema, Rais Dkt. Samia anapambana usiku na mchana, na hayupo tayari kuona sekta hiyo inatetereka, hali iliyomlazimu kuongeza bajeti sekta ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2022/2023 hadi shilingi Trilioni 1.24 mwaka 2023/2024.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga, wilayani Kahama, Waziri Bashe amesema,kazi iliyotukuka inayofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, inapaswa kuungwa mkono na watendaji wote.

“Rais Dkt. Samia hana deni Wizara ya Kilimo, anaipenda sekta hii,amefanya mengi, lengo likiwa ni kutaka matokeo mazuri sekta ya kilimo, haijawahi kutokea bajeti kutoka shilingi bilioni 294,hadi shilingi Trilioni 1.24.Sisi wasaidizi wake na watendaji tunao wajibu wa kufanya kazi usiku na mchana,”alisema Waziri Bashe

Ametumia fursa hiyo, kuwafikishia salamu za Rais Dkt. Samia, wakazi wa Kata ya Isagehe, na kueleza kuwa dhamira yake ya kukuza kilimo ni ya kudumu na ataendelea nayo katika kuinua hali ya wakulima nchini.

Amewataka wataalamu sekta ya kilimo, ikiwemo maafisa kilimo na ugani kuishi vijijini, kuhakikisha wanasaidia jamii waliyopo ili kuiwezesha sekta ya kilimo kuwa na tija na kuleta matokeo anayoyatarajia Rais Dkt. Samia.
Pia ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kuhakikisha mradi wa bwawa la umwagiliaji lililopo katika kijiji cha Malenge, Kata ya Isagehe, lenye ukubwa wa mita za ujazo 600,000,wenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 linajengwa.

Waziri Bashe pia amemshukuru Mzee Shija Lukinga, ambaye ni mmiliki aliyetoa eneo lake la ardhi bure ili kupisha mradi huo. “Hii ni taswira chache ya Mzee Shija kujitolea na ni kipaji cha kipekee.

"Bwawa hili linufaishe wakulima 427, mifereji isakafiwe kwa hekta 400 zilizobaki, tutumie wataalamu wa ndani katika ujenzi wa bwawa, ujenzi wa ghala na kinu na jina la mradi kuanzia sasa lisajiliwe kwa jina la Shija kutoka jina la awali la Malenge,”amesema Waziri Bashe.

Bashe ameongeza kuwa, tume itoe ushauri wa zana zinazohitajika katika uzalishaji ndani ya skimu hiyo.

“Mradi huu uwe na kilimo cha uhakika cha kuvuna hadi mara tatu kwa mwaka,”amesema Waziri Bashe.

Aidha, Waziri Bashe amewashukuru pia Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu,Barrick kwa kuwezesha mradi huo.
“Sisi kama Serikali tutakamilisha usakafiaji wa kilometa 12 zilizobaki,na Serikali itajenga hekta 400 za tuta zilizobaki,” ameongeza.

Ameeleza eneo hilo kutajengwa Kituo cha zana za Kilimo na ujenzi wa maghala kwa ajili uhifadhi wa mpunga.

“Ninamuomba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha,kufanya kikao cha ujirani mwema na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ili bonde la Manonga lilindwe kwa ajili ya miundombinu ya uzalishaji wa chakula, badala ya kujenga nyumba za wakazi. Tulinde ardhi ya kilimo,” amesema Waziri Bashe.

Katika hatua nyingine, Waziri Bashe ametembelea shamba la Serikali ya kijiji la Kisuke lililopo Kahama, na kuitaka ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha eneo hilo linapimwa, ili lipate hati na isome eneo la kilimo Isuke na wizara ya kilimo

Pia eneo hilo, litanufaika na mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), kwa watu wa kijiji na Bodi ya Pamba ifanye eneo hilo kuwa mradi mkubwa wa kuzalisha pamba.

“BBT hii wanufaika wawe ni wananchi kwa kukatiwa maeneo,hivyo itakuwa bbt ya wananchi wa kisuke na Serikali tutasimamia mradi huo na bodi ya pamba ifanye uwekezaji, ilete trekta na pawatila za kutosha na umwagiliaji wafanye utafiti wa ujenzi wa bwawa.

"Hivyo, wataalamu wa wizara,watu wa pamba, BBT, ASA, umwagiliaji muunde timu ya utafiti na Mkurugenzi zungumzeni na tarura barabara ya kuingia shambani ifunguliwe,wizara tutashirikiana mkihitaji,”amesema.
Kwa upande wa Meneja wa Mradi wa Tume ya Umwagiliaji Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Ebenezer Kombe, amesema bwawa la Shija litakuwa na mifereji mikuu na midogo ya kuingiza maji mashambani yenye urefu wa jumla ya kilomita 13 na eneo litakalotengwa kwa ajili ya kunywesha mifugo.

Mradi unatekekelezwa kwa ufadhili wa Kampuni ya Barrick kwa kushirikiana na Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news