Rais Dkt.Samia ziarani China kushiriki Forum on China-Africa Cooperation (FOCAC)

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini China kuanzia leo Septemba 2 hadi Septemba 6, 2024 kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa B. Nyanga.

Ameeleza kwamba, wakati wa ziara hiyo Rais Dkt. Samia atakutana na mwenyeji wake Rais wa China, Xi Jinping, kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano mzuri na wa kihistoria kati ya Tanzania na China ulioasisiwa miaka 60 iliyopita.

Marais hao wawili pamoja na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema watashiriki na kushuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano ya Uboreshaji wa Reli ya TAZARA

Pamoja na mambo mengine, miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele kwenye Mkutano wa FOCAC ni uendelezaji wa miundombinu, kukuza uwekezaji, uendelezaji wa viwanda, kilimo cha kisasa,amani na usalama.

Rais Dkt. Samia anatarajia kuwa miongoni mwa Wakuu wa Nchi watakaohutubia ufunguzi wa Mkutano wa FOCAC akizungumza kwa niaba ya Kanda ya Afrika Mashariki.

Pembezoni mwa mkutano huo, katika kukuza biashara na uwekezaji, Rais Dkt. Samia atakutana na makampuni na Wawekezaji kutoka China kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news