RC Kunenge amwapisha DC wa Rufiji, Luteni Kanali Komba

PWANI-Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakari Kunenge amehimiza ushirikiano miongoni mwa viongozi wa mkoa huo ili kurahisisha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Kunenge ametoa kauli hiyo Septemba 4, 2024, wakati wa hafla fupi ya kumwapisha mkuu mpya wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Faustin Komba, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Amesema,ushirikiano ni nguzo muhimu katika kufanikisha mawazo bora kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi na kupanga mipango ya maendeleo kwa kuzingatia uwezo na taaluma za watumishi mbalimbali.

"Huwezi kufanikiwa kama kila kitu unataka kionekane ni kazi yako pekee," amesema Mheshimiwa Kunenge.

Aidha, ameongeza kuwa changamoto za wananchi ni za aina mbalimbali, ambazo zinahitaji wataalamu tofauti kwa ajili ya kuzitatua.

Alisisitiza kuwa,ushirikiano utawezesha mipango bora ya maendeleo na kutatua changamoto hizo kwa ufanisi zaidi.

Kunenge aliwakumbusha viongozi wa mkoa kufanya kazi kwa mujibu wa mamlaka na majukumu waliyopewa, na kuhakikisha maamuzi wanayofanya ni sahihi ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

"Hata mtu akikuuliza majukumu yako ni yapi, uwe na uwezo wa kuyaelezea kwa ufasaha," alisisitiza Kunenge.

Vilevile, aliwataka viongozi hao kusimamia ipasavyo ulinzi na usalama pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo ni msingi wa maendeleo kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mheshimiwa Simon Nickson, aliwahimiza viongozi kufanya kazi kwa weledi ili kuleta matokeo chanya ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Faustin Komba, aliahidi kutekeleza majukumu yake mapya kwa kufuata sheria na kushirikiana na viongozi wenzake ili kuhakikisha utekelezaji wa sera za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news