DAR-Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kila Mwananchi anatumia Nishati Safi ya Kupikia.

“Mhe. Rais wakati anazindua Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 Mwezi Mei mwaka huu alitoa maagizo maalum kwa REA; kwakuwa tumefanya vizuri katika kusambaza umeme vijijini huku nako kwa kushirikiana na wadau wengine tuhakikishe asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi za Kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema Mhandisi Saidy.
Mhandisi Saidy alibainisha kuwa Wakala umeanza kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais kwa namna mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi za Kupikia kwa kuondokana na fikra kuwa bidhaa za Nishati Safi ni ghali ama si salama na kwamba chakula kinachopikwa kwa Nishati Safi hakina ladha.
“Tunaendelea kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kwamba suala la ladha ya chakula linategemea umahiri wa mpishi ama viungo vinavyotumika na sio nishati inayotumika kupikia,” alisema Mhandisi Saidy.
Mhandisi Saidy alisema,Wakala unaendelea kuwezesha upatikanaji wa Nishati Safi za Kupikia kwa kushirikiana na watoa huduma ambapo REA inawapa fursa watoa huduma kujitangaza ili kuwezesha wananchi wengi kufahamu uwepo wa teknolojia rafiki za nishati safi za kupikia.
Alibainisha kuwa, Serikali kupitia REA inatoa ruzuku ili kuwezesha wananchi wamudu kununua bidhaa za Nishati Safi za Kupikia na kujionea ubora wa bidhaa hizo kwa lengo la kuendelea kuhamasisha wananchi wengi wahame kutoka kwenye kutumia nishati zisizokuwa salama.
“Serikali imetoa ruzuku ili kila mwananchi aweze kumudu gharama; Mathalan kwenye mitungi ya gesi (LPG) na vichomeo vyake Serikali kupitia REA imeidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kitumike kusambaza Mitungi ya Gesi ya kilo 6 itakayonufaisha watanzania wapatao 452,445 kwa bei ya ruzuku,” alifafanua.
Mhandisi Saidy alibainisha kuwa, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya mia moja zianze kutumia Nishati Safi za Kupikia na kwamba katika utekelezaji wake, REA imeandaa miradi ya kufikisha bidhaa na teknolojia za Nishati Safi za Kupikia kwenye taasisi hizo.

Sambamba na hilo, Mhandisi Saidy alisema REA inafanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo linazalisha mkaa rafiki na kwamba REA inakwenda kuiwezesha STAMICO kununua mashine tatu za kuzalisha mkaa rafiki ili iweze kufikisha huduma kwenye maeneo mengi zaidi.
