REA yafikisha umeme Kijiji cha Nzinga Kibaoni,wagawiwa mitungi ya gesi

LINDI-Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Mhe. Francis Kumba Ndulane amewasha umeme katika Kijiji cha Nzinga Kibaoni Tarafa ya Njinjo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini. 

Pia, amepongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa namna ambavyo imeendelea kubadili vijiji kufanana na miji na pia kuweza kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kuwepo kwa kupitia nishati safi na salama.Mhe. Ndulane ameyasema hayo Septemba 21, 2024 alipokuwa akiwasha umeme na kugawa mitungi ya gesi katika Kijiji cha Nzinga Kibaoni.

Zoezi ambalo linakwenda sambamba na kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo amewaasa wananchi nchini kuhama katika matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia na kuhamia katika matumizi ya nishatisafi ya kupikia.

Mitungi hiyo ya gesi imegawiwa kwa wananchi kijijini hapo na Serikali kwa wajasiliamali, vijana na wanawake kupitia REA.Akielezea madhara yapatikanayo kwa matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa mifumo ya kiikolojia, magonjwa ya macho na mfumo wa kupumua pamoja na ukatili wa kijinsia na wananchi kukosa muda wa kushiriki shughuli za kijamii, kiuchumi na kimasomo.

Amewataka wananchi wa Kijiji cha Nzinga kuchangamkia fursa hiyo ya kuhama katika nishati isiyo salama na kujikita katika nishati safi ni rahisi kutumia ili kuokoa muda.
Pamoja na mambo mengine amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani alidhamiria kuhakikisha kuwa huduma ya nishati hususani umeme inapatikana kila mahali nchini.

Vilevile amewaomba wananchi kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais katika kuleta maendeleo nchini ikiwemo mawasiliano, maji,umeme pamoja na elimu.

Amewataka wananchi katika Kijiji cha Nzinga kuchangamkia fursa ya umeme wa uhakika ambapo fursa nyingi za kiuchumi zitapatikana na umeme usitumike kuwasha taa tu bali utumike katika kuhakikisha unabadili maisha ya wananchi kwa kufungua mashine za kusaga na shughuli nyinginezo za kiuchumi.
Akizungumzia mradi wa REA mzunguko wa pili katika Jimbo la Kilwa Kaskazini mradi amesema mradi ulikuwa na vijiji kumi na sita (16), lakini mpaka leo hii vijiji saba tayari vina umeme na vijiji vingine tisa (9) vitaunganishwa kabla ya tarehe 30 Novemba, mwaka huu. 

Nzinga ni kijiji kikubwa kuliko vyote katika Jimbo la Kilwa Kaskazini kina idadi ya watu 9,500 kwa mujibu ya sensa ya mwaka juzi kupatikana kwa huduma ya umeme katika kijiji hiki kitasukuma maendeleo katika vijiji vingine na jimbo zima Kilwa Kaskazini.

‘’Namshukuru Mkurugenzi Mkuu REA kwa kuweza kutekeleza miradi yenye tija na inayoleta matunda katika Jimbo letu la Kilwa Kaskazini na Wilaya nzima ya Kilwa na kuwataka REA kuhakikisha wanakamilisha miradi yote ya REA mzunguko wa pili ikiwemo miradi ya vitongoji kumi na tano (15),"amesema Mhe. Ndulane.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA),Mhandisi Hassan Saidy amesema, Kijiji cha Nzinga ni moja ya kijiji kinachopata umeme kupitia REA, lakini pia ndani ya Jimbo la Kilwa Kaskazini kwa mwaka huu vitongoji kumi na nne (15), vitapatiwa umeme amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuipatia fedha za kutosha REA ili kuweza kutekeleza miradi hii.‘’Nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu kwani Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni muasisisi barani Afrika na Tanzania ambapo ametoa maagizo kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wanahama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia na kuhamia katika nishati safi ya kupikia, ambapo jiko la gesi na mtungi unaouzwa kwa kiasi cha shilingi 45,000 wananchi vijijini watanunua kwa bei ya shilingi 20,000 huu ni mkakati mahsusi ambapo Serikali kupitia REA italipia kiasi kilichobaki,’’amesema Mhandisi Saidy.

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), itagawa takribani mitungi 450,000 nchi nzima na Wilaya ya Kilwa itapata takribani mitungi 3,500 na itagawiwa sawa kwa majimbo ya Kilwa Kaskazini na Kilwa Kusini.

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imegawa kiasi cha mitungi 231 katika vijiji vya Ndete Tarafa ya Kipatimo na kijiji cha Nzinga Kibaoni Tarafa ya Njinjo Katika Jimbo la Kilwa Kaskazini ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mahsusi wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa wananchi wanatoka katika matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia na kuhamia katika Nishati safi ya kupikia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news