NA LWAGA MWAMBANDE
NENO la Mungu kupitia Biblia Takatifu inatufundisha na kutusihi kuwa, hatupaswi kulipiza kisasi kwa yule aliyetufanyia ubaya.
Rejea, Warumi 12:19 neno la Mungu linasema kuwa, "Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena Bwana."
Kumbuka kuwa,kulipa kisasi kwa mambo uliyofanyiwa ambayo hayakupendezi unaweza kukabiliana na hasara nyingi.
Hivyo,usilipe kisasi kwa jambo lolote iwe masuala ya kidini,kifamilia,kikazi, mahusiano na majirani zako,kiuchumi au kibiashara.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, anayelipa kisasi hana shirika na Mungu. Endelea.
1. Mtu mwenye kubariki, ndiye atabarikiwa,
Mungu anamuafiki, tena anamuelewa,
Mabaya hayamfiki, wigo amezungushiwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
2. Hulipi baya kwa baya, hata unapokosewa,
Na tena huoni haya, mema watu kutendewa,
Wewe uko on faya, uzidi kubarikiwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
3. Si lawama kwa lawama, vibaya ukitendewa,
Bali lawama wa wema, mwingine arudishiwa,
Hilo jambo kwako jema, nawe utazidishiwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
4. Kuonesha mambo mema, ndicho mlichoitiwa,
Siyo kufanya dhuluma, vya watu kuchukuliwa,
Kwa Mungu ili kuvuma, ogopa kushitakiwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
5. Ukubwa kupendapenda, muweze kutumikiwa,
Huko si vizuri kwenda, mwaweza kufanyiziwa,
Kutumika mkipenda, ndivyo Mungu anogewa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
6. Iga kwake Yesu Bwana, alivyodharauliwa,
Hata walimtukana, kwa sana alikosewa,
Walakini hakuona, wawe wa kufanyiziwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
7. Kwake Mungu aliomba, wapate kusamehewa,
Kwa vile walivyoyumba, kesho waweze elewa,
Yeye amebaki mwamba, kwetu anaabudiwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
8. Tumeitwa kubariki, na Mungu mbarikiwa,
Kufanya hivyo ni tiki, enzini tunapatiwa,
Na kujaziwa riziki, bila ya kupungukiwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
9. Taka shirika na Mungu, uzidi kubarikiwa,
Baraka ziwe ni fungu, uzidi kuinuliwa,
Kwa kutofungwa na pingu, kwa watu kufanyiziwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
10. Kisasi ni chake Mungu, tunapaswa kuelewa,
Wewe lia kwa uchungu, hata ukisingiziwa,
Mwache awapige rungu, ndivyo unapiganiwa,
Anayelipa kisasi, hana shirika na Mungu.
(1 Petro 3:9, Mika 5:5, Marko 9:35)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602