DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameufunga Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Maji wa Nchi za Afrika, Carribean na Pacific uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Akifunga mkutano huo leo Septemba 13,2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere, Rais Dkt. Mwinyi amezisisitiza nchi wanachama kuendelea kushirikiana na kusimamia ipasavyo Sekta ya Uvuvi na Mazao ya Bahari kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi ameuelezea Mradi wa FiSHCAAP ulioendeshwa katika nchi kumi na mbili kwa mafanikio makubwa na kuwa nyenzo muhimu ya kupunguza uvuvi usio sahihi na uvunaji wa mazao ya bahari pamoja na kubadilisha mitazamo ya kiuchumi ya jamii katika nchi husika.
Amesisitiza kuwa, wakati umefika wa kuunganisha nguvu za pamoja,mbinu na maarifa yaliopatikana kupitia mradi huo kuimarisha sekta ya jvuvi pamoja na kuziongezea thamani bidhaa za Mazao ya Bahari.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,kasi ya ongezeko la watu katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kunabainisha kutakuwa na mahitaji makubwa ya upatikanaji wa samaki katika miaka ijayo yanayohitaji usimamizi endelevu wa bahari.
Halikadhalika Dkt.Mwinyi amesema Tanzania itaendelea kuidhirishia dunia kuwa mabadiliko ya mfumo wa chakula yanawezekana kwa kuwa na Uvuvi endelevu.
Rais Dkt.Mwinyi ameongeza kuwa, Tanzania kupitia Mpango wake Mkuu wa sekta ya Uvuvi wa 2021 hadi 2037 na Mpango Mkuu wa Uvuvi wa Zanzibar wa mwaka 2023 hadi 2038 pamoja na Mpango Mkuu wa Taifa wa Utekelezaji kuwa endelevu na wenye kuleta ufanisi katika kusimamia sekta ya Uvuvi na Mazao ya Bahari.