DODOMA-Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amesema Serikali inalitambua deni la Shilingi Bilioni 1.52 lililotokana na mapunjo ya mafao kutoka kwa waliokuwa wafanyakazi na madeni ya Wazabuni wa Mgodi wa Kiwira Coal Mine kabla ya ubinafsishaji.

‘’Mhe. Spika, uhakiki wa madeni hayo ulibaini madai ya wafanyakazi yalikuwa shilingi bilioni 1.024 kwa wafanyakazi 893 na madeni ya wazabuni ikiwemo watoa huduma ya ulinzi yalikuwa ni shilingi milioni 496 na kufanya deni lote kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.52,’’ amesema Dkt. Kiruswa.
Amefafanua kuwa, baada ya Chama cha Wafanyakazi Mgodini (TAMICO) kuwasilisha malalamiko ya mapunjo hayo Serikalini, Serikali ilifanya ukaguzi maalum kupitia kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba 2008 na baadaye Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (Internal Audit General) alihakiki madeni hayo Agosti, 2021.