DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za taasisi za kitaaluma za kimataifa zinazoonesha dhamira ya kushirikiana na Zanzibar kuijengea uwezo wa kielimu katika nyanja mbalimbali.
Ameyasema hayo leo Septemba 13,2024 alipokutana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Imperial cha Uingereza,Profesa Lam Wamsley na Ujumbe wake Ikulu ndogo iliyopo Mtaa wa Laibon jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,bado nchi inahitaji kupanua wigo wa kitaaluma katika juhudi za kuleta maendeleo ili kukuza uchumi na kuongeza maarifa na ujuzi wa watu wake.
Ameyataja maeneo ya biashara, afya, utafiti na teknolojia ya mawasiliano kuwa muhimu kwa nchi na kuelezea kuunga mkono nia ya Chuo Kikuu cha Imperial cha Uingereza ya kufungua milango ya ushirikiano wa kitaaluma na kuanzisha programu tofauti kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Suza.
Pia, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa Zanzibar imeendelea kuweka mkazo zaidi katika kuviimarisha Vyuo Elimu ya juu ili kuandaa Wataalamu katika sekta mbalimbali na kwamba bado inahitaji kuungwa mkono kimataifa.Ujumbe huo umekuja nchini kuangalia maeneo ya ushirikiano na hatimaye kuanzisha programu za mafunzo.