IRINGA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi (Mb) Isimani amesema Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imepanga kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Ilolo Mpya, wilaya ya Iringa katika Mwaka huu wa fedha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi (Mb) Isimani akiteta jambo na Mhe. Fundi Mihayo (Diwani wa kata ya Ilolo Mpya) katika Mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake kwenye Kata hiyo.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kutembelea Miradi ya Maendeleo na kufanya Mikutano ya hadhara katika katika vijiji vitano ambavyo ni Luganga, Magozi, Mkombilenga, Ukwega na Ilolo Mpya vilivyopo katika Jimbo la Isimani Mkoani Iringa leo tarehe 28/09/2024.
Amesema msingi wa maendeleo ni wananchi kujituma na mtu yeyote asipotoshe kwa kudai kwamba hakuna wananchi wanaojitolea kuleta maendeleo, naomba mshirikiane na viongozi wanaohimiza wananchi katika kujiletea Miradi ya Maendeleo.
“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassani imempendeza kujenga kituo cha afya na kwa sera ya Serikali kila kata inatakiwa kuwa na kituo cha afya,” alisema Waziri Lukuvi.
Wataalam wa (TASAF) watapita kuelezea namna kila kijiji kitakavyoshiriki katika ujenzi wa majengo ili kila kijiji kishiriki kikamilifu katika kukamilisha ujenzi wa majengo ya kituo cha afya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi (Mb) Isimani pamoja na watendaji mbalimbali katika picha alipotembelea eneo linalotarajiwa kujengwa kituo cha afya katika Kijiji cha Ilolo Mpya.
“Nawapongeza wananchi kwa miradi ya maendeleo lakini kuna mambo makubwa zaidi yanakuja ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Itunundu kwenda Iringa Mjini ambayo tayari Serikali imeshatangaza tenda, ikiwa ni sambamba na tenda ya ujenzi wa mfereji wa Magoze."
Kwa upande wake Afisa Uwezeshaji na Ufuatiliaji wa TASAF, Salim Mshana amesema majengo yanayotarajiwa kujengwa ni majengo 7 ili kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya.
Afisa Uwezeshaji na Ufuatiliaji wa TASAF, Salim Mshana akifafanua jambo kwenye Mkutano wa hadhara katika ziara ya Waziri Lukuvi alipotembelea kata ya Ilolo Mpya.Ujenzi utahusisha jengo la wagonjwa wa nje, jengo la mama na mtoto, jengo la maabara, jengo la upasuaji, jengo la kufulia nguo, jengo kuhifadhia maiti, na nyumba ya waganga ambayo itakuwa mbili kwa moja na njia za kutembelea za kuunganisha majengo hayo.