ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatekeleza mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, na tayari imefanikiwa kujenga masoko katika mamlaka zote za Serikali za Mitaa Unguja na Pemba.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa,Serikali imeanzisha utaratibu mpya wa kutumia asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuweka utaratibu mzuri wa kutoa mikopo kwa makundi maalum maarufu kwa jina la 4.4.2, ikimaanisha asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana, na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Halikadhalika, Rais Mwinyi ameeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo umeisaidia Serikali kuvuka malengo iliyojiwekea katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025 ya kuzalisha ajira mpya laki tatu kabla ya kukamilika kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amewataka ZSSF kupanga mipango madhubuti itakayowahakikishia wajasiriamali wanaochangia kwenye mfuko huo kupata mafao kwa wakati.