Serikali yawavutia kasi watumishi wazembe

NA LUSUNGU HELELA
Tabora

SERIKALI imesema haitawavumilia Watumishi wa Umma wenye kasumba ya kufanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa kushindwa kupata huduma bora.Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwenye Kikao kazi cha Watumishi wa Manispaa ya Tabora mara baada kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi, ikiwa ni ziara ya kimkakati ya kuwafuata watumishi katika maeneo yao ya kazi badala ya kuja Dodoma.

Amesema tabia hiyo imekuwa ikikwamisha azma ya Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuona Wananchi wanahudumiwa ipasavyo katika ofisi za Serikali.
Amewataka Watumishi hao kutambua kuwa suala la kutoa huduma bora kwa wananchi si hisani bali ni wajibu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu amezitaka Mamlaka za ajira na nidhamu kusimamia haki na stahiki zote za watumishi huku akizionya Mamlaka hizo kushauri ipasavyo bila kuwaumiza watumishi kwa lengo la kuwafurahisha viongozi wao.
Amesema ni jambo la aibu kuona Watumishi wakiwasilisha changamoto zao mbele ya Viongozi wa Kitaifa wanapofanya ziara katika maeneo yao ilhali changamoto hizo zingetafutiwa ufumbuzi katika ngazi ya wilaya au mkoa.

Amesema,kitendo hicho kinaonesha kuwa baadhi ya Watumishi hawawajibiki ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao.
"Haipendezi kuona Watumishi wakiwa hawatimizi wajibu wao wakitumia simu na kupiga soga muda wote kipindi cha muda wa kazi,"amesema Mhe.Sangu.

Sambamba na hilo Mhe.Sangu ametoa rai kwa Watumishi kujiepusha kutenda vitendo vitakavyopelekea kufukuzwa kazi huku akisisitiza kuwa mchakato kurudishwa kwenye utumishi wa umma ni jambo gumu.
Hivyo, Mhe.Sangu amewasihi watumishi wa Umma nchini kujiepusha vitendo hivyo,kwani mchakato wake wa kupata kibali cha kurudishwa unachukua muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news