NA VERONICA MWAFISI
KAIMU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Wakurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara pamoja na Waratibu wa Jinsia Ngazi ya Wizara kuweka mbinu za kuimarisha mfumo wa utoaji haki, kudhibiti uonevu, dhuluma, unyanyasaji na unyonyaji wa kijinsia pamoja na kuingiza masuala ya jinsia katika Mipango, Mikakati na Programu ya Wizara zao ili kuleta maendeleo endelevu.



Amesema,ujumuishwaji wa masuala ya jinsia ni muhimu sana maana ni chachu na huleta ufanisi na tija katika utendaji wa kazi. Aidha, huwawezesha watumishi wanaume kwa wanawake kutumia ujuzi, vipaji na vipawa walivyonavyo kutekeleza majukumu yao na kuleta taswira njema katika taasisi zao.
Amesema Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha Usawa wa Kijinsia katika Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja kuweka mazingira wezeshi yanayozingatia mahitaji ya kijinsia na hatua za makusudi (affirmative actions) ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi na majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi ili kuzifikia fursa na kujenga usawa kati ya wanawake na wanaume na kuwezesha utekelezaji wa lengo namba tano (5) la Malengo Endelevu ya Mwaka 2030 kufikia Usawa wa Kijinsia kwa asilimia 50.
Bw. Daudi ameishukuru Taasisi ya UONGOZI kwa kuendelea kutafsiri ndoto za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo kwa nyakati tofauti wameandaa programu za Uongozi kwa Wanawake awamu kwa awamu na kuwezesha kufanyika kwa Semina elekezi juu ya mwongozo wa ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma kwa Ngazi ya Wizara.
Semina hiyo ya siku mbili imeratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI.