NA DIRAMAKINI
SIMBA SC ya jijini Dar es Salaam imeendelea kujiwekea rekodi ya namna yake baada ya leo kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Ushindi huo umewafanya kwa mara ya sita kutinga hatua ya makundi katika mashindano ya CAF.
Hiyo inajumuisha mara nne katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika na mara mbili katika Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Ubabe wao wameuendeleza leo Septemba 22,2024 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli mtanange uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Cristovao Mabulu aliipatia Al Ahli Tripoli bao la kwanza dakika ya 17 kufuatia mlinzi wa kati Che Fondoh Malone kurudisha mpira wa kichwa.
Mpira ambao ulikuwa mfupi kwa mlinda mlango, Moussa Camara kabla ya kumkuta mfungaji.
Aidha,Kibu Denis aliwapatia Simba SC, bao la kusawazisha dakika 36 kwa mpira wa tiktak ya mguu wa kushoto baada ya kumalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Che Malone.
Leonel Ateba aliwapatia Simba SC bao la pili dakika ya 46 baada ya mlinzi wa kati Murad Hedhili kukosea kutoa pasi kabla ya kumkuta mfungaji.
Edwin Balua aliwapatia Simba SC bao la tatu dakika ya 90 kwa shuti kali nje ya 18 baada ya kupokea pasi ndefu kutoka nyuma kabisa.
Licha ya ushindi huo mnono chini ya Kocha Fadlu Davids,pia wamejikusanyia shilingi milioni 15 za goli la hamasa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.