ARUSHA-Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Eliud Sanga amewaonya watumishi, watoa huduma, waajiri na wanachama wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu kuacha mara moja kwa kuwa bodi yake haitavumilia hilo.

“Kwa watumishi wa mfuko, wanachama na watoa huduma wasio waaminifu wanaojihusisha na udanganyifu waache mara moja, hatuna uvumilivu katika kuona yeyote akijinufaisha kupitia huduma zinazotolewa tunahitaji kuona mfuko ukiwa hai na ukitoa huduma nzuri,” amesisitiza.
Aidha, ameitaka Menejimenti kuhakikisha inaimarisha mifumo yake ya ndani ili iweze kubana mianya yote ya udanganyifu na iwezeshe utoaji wa huduma bora na kwa wakati.
Akizungumzia utendaji kazi wa watumishi, amewataka kujipima wenyewe na kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia maadili na taratibu zote zilizopo na kuachana na tabia za kuweka makundi mahala pa kazi.
“Tusitengeneze makundi ndani ya mfuko wetu, tengenezeni mfumo mzuri wa utendaji kazi ili muweze kutoa huduma bora kwa wadau wetu na matarajio ya Serikali yaweze kufikiwa,” amesema Mwenyekiti wa Bodi NHIF.

Amewataka watumishi kumpa ushirikiano na kumtumia vizuri katika uboreshaji wa huduma kwa kuwa anao utaalam wa kutosha katika eneo la hifadhi ya jamii.

“Naomba kuweka wazi kwamba sina uvumilivu (zero tolerance) kwenye masuala ya udanganyifu na uzembe nitasimamia kuhakikisha tunaongeza wigo wa wanachama, tunatoa huduma bora kwa wanachama wetu. Nitasimamia matumizi ya TEHAMA, tumeanzakubana matumizi ili tupunguze nakisi ya Mfuko.

Akizungumzia maandalizi ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, amesema Mfuko umeanza matayarisho hasa katika eneo la utoaji wa elimu kwa umma, mifumo itakayotumika katika kuandikisha wanachama, kukusanya michango na kuchakata madai.
“Tumeweka mipango yetu vizuri katika kutekeleza hili la bima ya afya kwa wote, tunajua matarajio ya Serikali katika jambo hili, hivyo nikuahidi kuwa tutafanya kazi kwa kujituma ili kufanikisha azma ya serikali," amesema Dkt. Isaka.
