Sudan Kusini yaongeza kipindi cha mpito,yaahirisha uchaguzi

NA DIRAMAKINI

OFISI ya Rais ya Jamhuri ya Sudan ya Kusini, chini ya Uenyekiti wa Rais Salva Kiir Mayardit, imetangaza kuongeza muda wa kipindi cha mpito nchini humo kwa miaka miwili.
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit.

Sambamba na kuahirisha uchaguzi ambao awali ulipangwa kufanyika Desemba, 2024 badala yake utafanyika Desemba 22, 2026.

Mshauri wa Rais kuhusu Usalama wa Taifa, Mhe. Tut Gatluak aliwaeleza waandishi wa habari Septemba 13,2024 jijini Juba kuwa, nyongeza hiyo ni fursa ya kutekeleza itifaki muhimu zilizosalia.

Ni katika Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Mzozo katika Jamhuri ya Sudan Kusini (The Revitalised Agreement on the Resolution of the Conflict in the Republic of South Sudan (R-ARCSS).

Miongoni mwa mambo hayo ni mchakato wa katiba ya kudumu, sensa na usajili wa vyama vya siasa.

Kwa upande wake, Waziri wa Masuala ya Baraza la Mawaziri, Dkt. Martin Elia Lomuro alisema nyongeza hiyo ni kutokana na mapendekezo ya taasisi za uchaguzi na sekta ya usalama.

Akitaja majukumu muhimu yanayosubiri kutekelezwa kwa ufanisi wa uchaguzi, na kulazimisha kucheleweshwa, akisema kuna haja ya muda wa ziada kukamilisha kazi muhimu kabla ya uchaguzi.
Waziri Lomuro pia aliuhakikishia umma kwamba,serikali itaendelea kufanya kazi katika kipindi hiki kirefu.

Aidha, Waziri huyo alisisitiza kuwa Serikali haitavunjwa na itaendelea kufanya kazi kama kawaida wakati taasisi hizo zikiendelea kukamilisha masharti yake.

Ofisi ya Rais pia imesisitiza kwamba,miezi iliyosalia ya kipindi cha mpito cha sasa itatumika kukusanya fedha, zinazolenga utekelezaji mzuri wa makubaliano ya amani yaliyohuishwa.

Mpango huo, Dkt. Lomuro alisisitiza kuwa ni muhimu kwa ajili ya kufikia amani na utulivu wa muda mrefu nchini Sudan Kusini.(SSSH)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news