NA GODFREY NNKO
AFISA Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw.Kadari Singo amesema, anatarajia Watanzania wengi watakisoma Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake) kwani kimeandikwa kwa lugha fasaha ya Kiswahili.
Singo ameyabainisha hayo leo Septemba 30,2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho ambacho kinazinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Vile vile, Singo ameishukuru Familia ya Hayati Edward Moringe Sokoine kwa kuwa sehemu ya Mradi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Viongozi wa Kitaifa nchini na Barani Afrika.
"Na pia kwa kuwa waangalifu kwa kuhifadhi vema nyaraka mbalimbali zinazohusu maisha ya hayati Edward Moringe Sokoine."
Amesema kuwa, kazi ya uandishi wa vitabu vya viongozi huwa inachukua muda mrefu kwa kuwa inahusisha vikao, mahojiano mbalimbali kwa ajili ya kukusanya na kupitia na kuthibitisha taarifa.
"Tofauti na vitabu vya Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa,ambavyo viliandikwa na wao wenyewe kabla ya kutangulia mbele ya haki.Kitabu cha Sokoine kinaandikwa takribani miaka 40 tangu kifo chake kwa kukusanya taarifa rasmi za Serikali sambamba na kufanya mahojiano na viongozi mbalimbali waliowahi kufanya kazi naye kwa namna moja ama nyingine.
"Kutokana na muhusika kutokuwepo, zoezi la kukusanya taarifa lilihusisha sana familia ya Hayati Sokoine, na kwa kweli wametoa ushirikiano wa kutosha, tunawashukuru sana."
Amesema, baada ya majadiliano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Familia ya Hayati Edward Sokoine, Taasisi ya Uongozi na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine iliafikiwa kitabu hicho kiandikwe kwa lugha fasaha ya Kiswahili.
"Ni kwa lengo la kuwafikia Watanzania wengi iwezekanavyo,aidha uamuzi huu unaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za Serikali,Kitaifa na Kimataifa. Ni matumaini yetu, kwamba Watanzania wengi watapata fursa ya kukisoma kitabu hiki.Ili kujiongezea maarifa na kuifahamu vema historia ya Taifa letu, na Afrika kwa ujumla.
Mtendaji Mkuu huyo amemweleza Rais Dkt. Samia na washiriki wa hafla hiyo kuwa, Taasisi ya Uongozi inaelekeza shukurani zake kwa wale wote ambao walishiriki kwenye mchakato wa uandishi na uchapaji wa kitabu hicho.
Pia, amewashauri viongozi mbalimbali walioko madarakani kujiwekea utaratibu wa kuandika vitabu vyao kupitia majukumu wanayoyatekeleza kila siku ili kutoa wepesi wa kumbukumbu zao kupatikana kiurahisi pindi wanapostaafu.