NA DIRAMAKINI
NDANI ya Charles Konan Banny Stadium jijini Yamasoukro nchini IvoryCoast, timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefanikiwa kuzoa alama tatu.
Ni baada ya Septemba 10,2024 kuwacharaza wenyeji Guinea mabao 2-1 katika mchezo wa Kundi H wa hatua ya makundi kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitakazofanyika nchini Morocco.
Mchezo huo ambao awali ulionekana mgumu kwa pande zote, wenyeji walianza kutupia bao la kwanza kipindi cha pili dakika ya 57.Ni kupitia bao ambalo lilifungwa na Mshambuliaji wa Klabu ya Ligue 1 ya Lille nchini Ufaransa,Mohamed Bayo.
Bao ambalo dakika ya 61 lilisawazishwa na kiungo mshambuliaji wa Azam FC,Feisal Salum 'Fei Toto'. Licha ya pande hizo mbili kuendelea kutoshana nguvu, Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya Abbas alifunga hesabu dakika ya 88.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars imefikisha alama nne baada ya mechi mbili ikisalia nafasi ya pili kwenye Kundi H alama mbili nyuma ya vinara DR Congo.
Aidha, katika kundi hilo nafasi ya tatu inashikiliwa na Ethiopia kwa alama moja huku Guinea wakiburuza mkia kwa alama sufuri baada ha mechi mbili.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewapongeza Taifa Stars kwa ushindi huo.
"Hongera kwa vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi wenu dhidi ya Guinea katika hatua ya makundi kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
"Tunawaunga mkono na kuendelea kuwatakia kila la kheri katika hatua hii muhimu,"ameandika Rais Dkt.Samia.