DAR-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) imetunukiwa tuzo na JamiiForums kwa kuwa mstari wa mbele kupokea taarifa, kero au malalamiko ya wananchi yenye viashiria vya rushwa zinazotumwa kupitia majukwaa mbalimbali ya Jamii Forums ikiwemo Fichua Uovu na kuyafanyia kazi.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu,Crispin Francis Chalamila tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa wa taasisi hiyo, Bi.Sabina Seja kutoka kwa Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania, Christine Grau.
Bi.Seja amesema, "Tuzo hii ina maana kubwa sana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambayo inafanya kazi na wadau mbalimbali lwani jukumu la kuzuia vitendo vya rushwa ni la kila mwananchi.
"Jamiiforums wanapokea taarifa mbalimbali kupitia majukwaa waliyonayo, hivyo majukwaa haya yamekuwa ni fursa kwa TAKUKURU kufanya kazi kwa pamoja na wadau mbalimbali kupitia njia ya kidijitali kwenye majukwaa hayo.

"Kwa hiyo majukwaa haya yanaweza kuchangia katika pande mbili, sehemu ya kwanza yanachangia katika uzuiaji pale ambapo taarifa inayotolewa inawezekana ni viashiria tu vya rushwa, lakini vitendo vya rushwa havijatendeka.
"Lakini,vile vile wakati mwingine vitendo vya rushwa vimeshatendeka, hivyo TAKUKURU inachukua hatua za kisheria kuweza kupambana na vitendo vya rushwa katika eneo hilo."
Bi.Seja amesema, majukwaa ya namna hiyo yameongeza wigo wa ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.
Tags
Habari
Jamiiforums
Programu Rafiki ya TAKUKURU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania