MTWARA-Mamia ya wananchi kutoka kata mbalimbali zilizopo Tarafa ya Mikindani wamejitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi wa tamasha la michezo ya asili (bao na draft) lijulikanalo kama MTONYA FESTIVAL.
Tamasha hilo limeandaliwa na Diwani wa kata hiyo, Mhe. Shadida Ndile ambaye ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikidani katika Viwanja vya Ofisi ya Kata hiyo na kuahidi kuwapatia zawadi nzuri washindi wa michezo hiyo.
Mhe. Ndile amesema kuwa, ameanzisha tamasha hilo ili kutimiza nia yake ya kuendeleza sekta ya michezo ndani ya Manispaa na kuleta furaha kwa wanajamii mara baada ya shughuli ya kutwa nzima ya kujitafutia kipato huku akiamini kuwa michezo inaimarisha afya na inaleta ajira.
Ameendelea kusema kuwa, ameanzisha tamasha hilo pia ili kuhabarishana juu ya uwepo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024 hapa nchini.
Aidha,Mstahiki Meya amekabidhi seti ya jezi ya Mpira wa miguu na Mpira mmoja Kwa madereva bodaboda na amezitaja zawadi zitakazotolewa kwa washindi wa mashindano hayo ni pamoja na mbuzi mmoja kwa mshindi wa kwanza wa michezo yote, fedha shilingi elfu hamsini (50,000) kwa mshindi wa pili na shilingi elfu thelathini (30,000) kwa mshindi wa tatu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliohudhuria Kwenye tamasha hilo wamempongeza Diwani huyo kwa kuendeleza michezo Katika Kata yake na wameahidi kushiriki kikamilifu Kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.