NA DIRAMAKINI
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini (ICTC),Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga amesema kuwa, Tanzania ni nchi ya 25 duniani kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Dkt. Mwasaga ameyasema hayo katika mahojiano kupitia kipindi cha 360 cha Clouds TV jijini Dar es Salaam.
ICT ni taasisi ya umma chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, yenye jukumu la kukuza na kuendeleza maendeleo ya TEHAMA hapa nchini.
Pia, ina wajibu wa kutathmini utekelezaji wa mikakati mbalimbali na kutoa ushauri pamoja na muelekeo wa wa utekelezaji wake.
"Ukiangalia vipimo mbalimbali vinavyopima kuhusiana na mambo ya TEHAMA duniani, sisi tunafanya vizuri.
"Huko duniani, tunaheshimika kwa mambo mengi kwa mfano katika kutoa huduma za Serikali, Tanzania ni kati ya nchi bora 25 duniani.
"Kwa hapa Tanzania, huduma nyingi unaweza kuzipata kwa mtandao, kama siyo zote, bili...tena hata ukiwa nje ya nchi unaweza uka-clear bila shida yeyote.
"Kwa hiyo, tuna mafanikio makubwa na hizo huduma haziwezi zikafanya vizuri kama mambo ya usalama wa mtandao hauko vizuri.
"Japokuwa, usalama wa mtandao ni changamoto ambayo ni endelevu. Lakini, hali ni nzuri na ndiyo maana tumepata hiyo nafasi (kuandaa kongamano la Kimataifa) na kuna vitu vingine vingi wakitupima sisi tunaenda vizuri sana.
"Hasa kutokana na hicho, ndiyo maana kuna mashindano ya Afrika ya Vijana ya Akili Mnemba na Mambo ya Roboti kwa mara ya kwanza Afrika yanafanyika hapa Tanzania.
"Ni kwa mara ya kwanza, kwa hiyo sisi tuko vizuri ila ninajua wananchi wanataka tuwe vizuri zaidi.
"Hilo jambo ninalichukulia very positive kwetu,sisi pia Tanzania kila Oktoba tunakuwa tuna kongamano letu la mwaka la TEHAMA ambalo kauli mbiu ya sasa hivi 'Ni Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Roboti ili kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi na Kijamii'.
"Kwa hiyo, tunaangalia kila kitu kinachohusiana na hilo jambo ili liende vizuri. Kile ambacho mliona bungeni ile ilikuwa tu tuna test mitambo.
"Lakini, ukiangalia lile jambo lilitupa heshima kubwa sana kwa sababu ni watu wachache sana wanaweza kuwa na uwezo wa kujiamini kupeleka teknolojia kama ile bungeni ikakubalika.
"Kwa hiyo ni kitu ambacho tumefanya mara ya kwanza na kimefanya vizuri. Endelea kutazama video hapa chini kwa taarifa zaidi;