LAS VEGAS-Tanzania na taasisi mbalimbali za Marekani zimekutana na kujadili kuimarisha ushirikiano baina ya Mataifa hayo mawili katika uendelezaji wa Madini Mkakati na Muhimu katika kikao maalum baina ya wataalam wakati wa Maonesho ya Madini jijini Las Vegas nchini Marekani mapema wiki hii.
Katika kikao hicho kilichofanyika Septemba 24, 2024, Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa akiambatana na wataalamu kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake ambako kiliongozwa na Katibu Msaidizi wa Masoko ya Kimataifa na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Biashara za Mambo ya Nje Marekani Arun Venkataraman.
Katika kikao hicho, Serikali ya Marekani kupitia Wakala wa Biashara na Maendeleo wa Marekani (USTDA) iliahidi kuisaidia Tanzania kwa kuwajengea uwezo wataalam wake kwa kuwapeleka nchini Marekani kujifunza teknolojia za kisasa za uendelezaji wa madini, lakini pia walikubaliana kusaidia Tanzania katika uanzishaji wa maabara ya kisasa ya madini na kuhakikisha kwamba wataalam wa Tanzania wanapata mafunzo ya hali ya juu.
Aidha, Serikali ya Tanzania imeombwa kukamilisha taratibu za kujiunga na Ushirikiano wa Usalama wa Madini Mkakati (MSP), ambao unajumuisha nchi kadhaa kama vile Marekani, Canada, Ujerumani, na Uingereza, ili kushirikiana katika kupanga mikakati ya kuendeleza madini mkakati duniani. Tanzania kupitia Wizara ya Madini imeonyesha dhamira ya kukamilisha taratibu hizo kwa ajili ya kujiunga na MSP.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kiruswa alibainisha mpango wa Tanzania kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia ndege ili kupata taarifa za kina za jiolojia huku akihimiza ushirikiano kati ya Serikali za Tanzania na Marekani kupitia makampuni ya madini ya nchi hizo mbili ili kuendeleza miradi ya madini mkakati na muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa nishati safi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na wataalam wa sekta ya madini kutoka taasisi tofauti za Marekani, wakiwemo Olimar Rivera Noa, Cornelius Gyamfi, Derek Schlickeisen, Jasmine Braswell, Mark E. Klein, na Thomas R. Hardy.
Katika hatua nyingine, Septemba 25, 2024, Dkt. Kiruswa alikutana na kampuni ya Vijana TZ Industries ambayo ni ya kitanzania inayojihusisha na Uchimbaji wa Madini ya Nakshi maeneo ya Ntyuka, Dodoma. Kampuni hiyo ilieleza mpango wake wa kuhamasisha vijana katika sekta ya uongezaji thamani wa madini, ambako Dkt. Kiruswa alisifu juhudi hizo na kuzihusisha na mpango wa serikali wa "Mining for Brighter Tomorrow" unaolenga kuendeleza vijana kwenye sekta ya madini kwa kuwapatia leseni na mitaji.
Katika maonyesho hayo, Dkt. Kiruswa alitembelea mabanda ya kampuni mbalimbali kujifunza teknolojia mpya zinazotumika katika utafiti na uchimbaji wa madini, vifaa vya maabara, na teknolojia za utunzaji wa mazingira.
Maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa Tanzania kujifunza na kutengeneza ushirikiano wa kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya madini nchini.