Tanzania na Saudia zaingia makubaliano kudhibiti uhalifu

RIYADH-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati ya makubaliano na Serikali ya Saudi Arabia makubaliano ambayo yanaenda kugusa sekta mbili muhimu za usalama ikiwemo udhibiti wa makosa mbalimbali ya uhalifu kwa kutumia utaalamu na teknolojia ya hali ya juu kwa Jeshi la Polisi.

Sambamba na udhibiti wa majanga mbalimbali ikiwemo moto,ajali za bararani,maporomoko kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi(kulia) akisaini hati ya makubaliano kati ya nchi yake na Serikali ya Tanzania katika kushirikiana na udhibiti wa matukio ya uhalifu kupitia Jeshi la Polisi na majanga mbalimbali kupitia Jeshi la Zimamoto.Makubaliano hayo yamesainiwa nchini Saudi Arabia.

Hati hiyo ya makubaliano kwa upande wa Tanzania imesainiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni na upande wa Serikali ya Saudi Arabia imesainiwa na Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi huku pande zote mbili zikionyesha nia ya kubadilishana uzoefu na vifaa mbalimbali ikiwemo vifaa vinavyotumia teknolojia katika udhibiti wa matukio ya uhalifu.

‘Nachukua fursa hii kumshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al -Saudi kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika ziara hii ambayo leo hii imepelekea kukamilisha uwekaji wa saini kwenye hati za makubaliano mbili.

"Moja ikihusisha upande wa Jeshi la Polisi ambapo serikali mbili hizo zinaenda kushirikiana katika kupambana na uhalifu lakini hati ya pili inahusu mashirikiano kwenye Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji na tumezisaini leo hapa na zinakwenda kufungua milango ya kuweza kushirikiana kwa mapana zaidi katika maeneo hayo mawili.

"Hati hii ambayo tumesaini leo itakwenda kufanya sasa nchi yetu kupitia Jeshi la Polisi kuweza kufaidika na fursa mbalimbali za mashirikiano ikiwemo katika kujenga uwezo wa askari wetu katika maeneo mbalimbali na kubadilishana uzoefu na teknolojia.

"Nimefarijika kuona serikali ya Saudi Arabia imeweka msisitizo katika maeneo ambayo hata sisi tumeweka nguvu kuimarisha matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kutoa huduma bora kwa wananchi,"amesema Waziri Masauni.

Waziri Masauni pia aligusia usalama wa kimtandao ambapo alisisitiza uwepo wa kipengele hicho katika hati ya makubaliano ili kuweza kudhibiti uhalifu wa mitandaoni ambao hivi sasa umeanza kushika kasi nchini.

"Tumeona wenzetu wameweza kuimarika sana katika matumizi ya teknolojia kudhibiti uhalifu wa kimtandao hivyo ni Imani yangu kwamba kupitia mashirikiano ambayo tumesaini kwenye hati ya makubaliano tunakwenda kufanikisha dhamira njema ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuimarisha jeshi letu la polisi katika eneo hilo.

"Kama mnakumbuka Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi sana kiasi cha dola za kimarekani milioni mia moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa mbali ya vifaa vingine ambavyo tayari vishaingia mwaka huu ambavyo vinahitaji askari wetu wawe na uwezo na uweledi wa kuvitumia sambamba na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao tayari walishaanza kupokea magari."

Akizungumza kwa upande wa Serikali ya Saudi Arabia,Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi alisema wapo tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kudhibiti matukio ya uhalifu huku akigusia uhalifu mbalimbali ulivyodhibitiwa nchini Saudi Arabia ambapo kila mwaka maelfu ya waumini wa dini ya kiislam na wageni kutoka mataifa mbalimbali hufika nchini humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news