NA GODFREY NNKO
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Kimataifa wa Merck Foundation Africa Asia Luminary ambapo washiriki kutoka mataifa 70 watajumuika pamoja jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt.Dorothy Gwajima akiwa ameambatana na Prof. Dkt. Frank Stangenberg Haverkamp,Mwenyekiti wa Merck Foundation na Seneta,
Dkt. Rasha Kelej, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation ameyasema hayo leo Septemba 18,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Dkt.Gwajima alikuwa akizungumzia kuhusu mkutano wa 11 wa Taasisi ya Merck Foundation ambao utafanyika nchini kuanzia Oktoba 29 hadi 30,2024.
Mkutano huo utafanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema, mkutano huo utaambatana na mkutano mwingine wa nchi ambazo wenza wa Marais wake watashiriki kwenye mkutano huo wa 11 na utajumuisha waandishi wa habari za afya kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Dkt.Gwajima amesema, mkutano wa Merck Foundation Africa Asia Luminary ambao unafanyika kwa mara ya 11 na mara ya kwanza nchini Tanzania, mikutano 10 iliyotangulia ilifanyika katika nchi za Ujerumani,Kenya, Ivory Coast, Misri, Mauritius,Senegal, Ghana, Zambia, Umoja wa Falme za Kiarabu na India.
"Kufanyika kwa mkutano huu nchini Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kunatokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan aliyeridhia ombi la taasisi hiyo kuwa mkutano huo ufanyike hapa nchini.
"Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali ombi hilo, hivyo kuwezesha Tanzania kupata heshima hiyo kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa Kimataifa kwa mara nyingine.
Amesema, Taasisi ya Merck Foundation ilipendekeza kufanya mkutano huo Tanzania kutokana na sababu kadhaa.
Mosi, Dkt.Gwajima amesema, ni jitihada za wazi za Serikali ya Awamu ya Sita na awamu zilizopita za kuwekeza katika sekta ya afya.
Uwekezaji huo ni pamoja na afya ya mama na mtoto, hivyo kuifanya Tanzania kufanya vizuri katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Kimataifa yakiwemo Milenia na maendeleo endelevu.
Pili, Dkt.Gwajima amesema,Tanzania pia imechaguliwa kutokana na mazingira mazuri ya amani na utulivu.
Kutokana na sifa hiyo,washiriki wa mkutano huo hususani viongozi mbalimbali watapata nafasi ya kutekeleza jukumu la kushiriki kwenye mkutano huo kwa amani na utulivu.
Jambo la tatu, Dkt.Gwajima amesema ni uongozi bora na wa kupigiwa mfano wa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema, Rais Dkt.Samia ameendelea kupaisha Diplomasia ya Tanzania ikiwemo Diplomasia ya Mikutano kama hiyo ya Kimataifa.
Katika hatua nyingine, Dkt.Gwajima amesema, mkutano huo unaratibiwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi ya Merck Foundation.
"Mkutano huu utafunguliwa Oktoba 29,2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kama mgeni rasmi wa mkutano huo."
Merck Foundation ni taasisi ya uhisani yenye makao makuu yake Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa ufumbuzi bora na usawa wa huduma za afya katika jamii, kujenga huduma za afya na uwezo wa utafiti wa kisayansi.
Vilevile kuwawezesha watu katika masuala ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kwa lengo maalum hususani wanawake na vijana.
Mkutano wa Merck Foundation Africa Asia Luminary hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Bara la Afrika na Asia.
Mikutano hiyo kwa kawaida huwa inawaleta pamoja watoa huduma za afya 6,000,watunga sera,wanataaluma,watafiti na wanahabari wa afya kutoka nchi zaidi ya 70.
Ni nchi zinazozungumza Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kihispania ambao hushiriki kwa njia ya ana kwa ana au kupitia mitandao.
Dkt.Gwajima amesema, washiriki wa mikutano hiyo huwa wananufaika na mikutano muhimu ya kielimu na maendeleo ya kijamii kutoka kwa wataalamu wa Kimataifa.
Ni katika masuala ya magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari,uzazi,huduma ya afya ya uzazi, dharura za watoto,saratani, afya ya wanawake.
Pia,huduma za kuzuia magonjwa ya moyo, huduma za wagonjwa mahututi, changamoto ya upumuaji, afya ya akili, tiba ya ganzi na mengineyo.
Amesema, lengo ni ili kuchangia katika uboreshaji wa usimamizi wa magonjwa, kugundua mapema, kuzuia, kujenga uwezo wa huduma za afya na kuboresha huduma ya upatikanaji wa afya bora ikiwemo huduma za afya zenye usawa.
Mwenyekiti wa Merck Foundation, Prof. Dkt. Frank Stangenberg Haverkamp amesema, wakfu huo utaendelea kusaidia katika kuendeleza na kutekeleza mipango thabiti ya kudhibiti na kuzuia saratani na magonjwa mengineyo.
Pia, wataendelea kutoa jukwa mahususi kwa wataalam wa afya, watunga sera wakiwemo wataalamu mbalimbali kutoka Afrika na Asia kushiriki ujuzi na uzoefu wao katika masuala ya afya na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Seneta,Dkt. Rasha Kelej ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation amesema, mbali na kuendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa afya, wakfu huo utaendelea kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika, Asia na nchi zinazoendelea.
Amesema, wataendeleza huduma za afya,kuwajengea uwezo wanahabari za afya ili waweze kuyatumia majukwaa na vyombo vyao vya habari kutoa elimu kuhusu masuala ya afya.