TANZENJ na SUZA wajadiliana kuwezesha Wanadiaspora kubadilishana utaalamu na vijana Zanzibar

ZANZIBAR-Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Uwekezaji ya TANZENJ, Bw. Suwedi Yunus Abdallah amefanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d Haji Makame kwa ajili ya kuwaleta Wazanzibari wanaoishi Ughaibuni kubadilishana utaalamu na vijana wa Zanzibar katika uwekezaji kwenye fani za kitaalamu na kitaaluma.
Mazungumzo hayo yalifanyika Septemba 3,2024 katika ofisi za makao makuu ya Chuo hicho huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema, kuna vijana wengi wako nje walio tayari kujitolea kwa vijana wazawa kwa kufanya kazi sambamba na kuwapa elimu itakayowasaidia kujiimarisha kiuchumi.

Abdallah ambaye pia amepata uzoefu wa kufanya kazi katika shirika linaloshughulikia masuala ya wakimbizi na kuishi katika nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya amesema ameona kuna mahitaji makubwa ya utaalamu kwa vijana kwenda kubadilishana uzoefu wenzao ughaibuni.

Mtaalamu huyo alisema, anaamini vijana wazawa wakiwaona wanadiaspora wamefanya vitu vikubwa kwenye nchi wanazoishi au hata hapa nyumbani na wao watashawishika kubuni mambo makubwa ya kutambuliwa kitaifa na kimataifa.

"Nataka kuiunganisha sekta ya uwekezaji na Serikali kwa watu wenye nia ya kuwekeza na kuleta tija kwa vijana na nchi yetu maana wapo wengine wababaishaji,’’alibainisha.

Alifahamisha kuwa,amewapata vijana walioko tayari kuja nchini ambao wana uzoefu katika miradi ya maji, kilimo, michezo na mbolea na masuala ya afya na hivi sasa nimekuwa natafuta namna gani naweza kufanya kazi na vyuo vikuu.

Aliongeza kuwa, yeye anatumia ushawishi wa kuwakaribisha nchini kwa kufanya kazi na taasisi zinazohusiana na utaalamu bila ya kuingiza fedha mfukoni kuwaleta wanadiaspora hao ambapo vijana wazawa 30 wamepata fursa ya kufundishwa masuala ya IT hapa nchini.

Aidha, amefanya mazungumzo na wizara na taasisi kadhaa za Serikali kuangalia maeneo gani wanaweza kushirikiana kwa njia ya kuwatumia wanadiaspora walio tayari kutoa mchango kwa vijana na nchi yao.

‘’Vijana wengi hawana ubunifu,lakini wana vipaji ambavyo vinahitaji kuamshwa na vikiibuliwa kutakuwa na wataalamu wengi ambao watatumika katika miradi mbalimbali badala ya kuwatumia wageni kutoka nje pekee,” alisema.

Naye Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Haji ameridhishwa na jitihada za mwanadiaspora huyo na kueleza kuwa SUZA ina maeneo mengi ambayo inahitaji kuongezewa nguvu kwa vijana kupewa ujuzi zaidi licha ya kuwepo ushirikiano mkubwa na taasisi nyengine za elimu za ndani na nje.

‘’Nimefurahia kuingiza wazo la Diaspora kwenye vyuo vikuu,kwani tuna mahitaji mengi ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi na elimu nchini,’’alisema Prof. Makame.

Aliyataja miongoni mwa maeneo hayo kuwa ni utafiti, kuandika miradi ya kukiwezesha Chuo kupata miradi na fedha, miundombinu hasa kwa eneo la chuo la hekta 64 ambalo linatarajiwa kuwa namabadiliko makubwa ya uwekezaji wa miundombinu, uchumi wa buluu, kilimo na afya.

Katika hatua ya awali, wana SUZA watafaidika na ziara ya mwanadiaspora aliyewahi kuwa kiongozi wa Jumuia ya Diaspora ya Uingereza kwa kupata mtaalamu wa kuwafundisha masuala yanayohusiana na IT.

Aidha, katika mazungumzo hayo, walikubaliana kuandaa hati ya makubaliano ili kuweka utaratibu maalum wa kualika wageni na kufanya kazi za kujitolea chini ya mwamvuli wa Diaspora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news