TANZIA:Safari ya mwisho ya Raymond Moyo Isaac Anderson Mwamusiku huko Maryland nchini Marekani

*Ni mnyakyusa wa Usale,Kyela mkoani Mbeya

*Mwili wake kuletwa nchini wiki ijayo kwa maziko

MARYLAND/DAR-Yalikuwa majira ya usiku mwingi,lakini kwa Raymond huo ulikuwa ndiyo muda wa kawaida wa kutoka kazini siku zote.Baada ya kutoka kazini alikuwa akiendesha muda mrefu kurejea nyumbani kwake.Alikuwa anaishi katika mji Columbia,ambayo ni sehemu ya Jiji la Baltmore,jimbo la Maryland nchini Marekani.Ameishi mjini hapo kwa takriban miaka 16, akiwa mkazi wa nchi hiyo mwenye Ukazi maalum wa kiwango cha Green Card.

Siku hiyo aliendesha gari lake aina ya Subaru Imprezza nyeupe,mpaka alipofika mahali njiani mwili ukawa umechoka.
Akaamua kupaki gari kwa muda kidogo hapo ili apumzike kwani alikuwa anajisikia usingizi pia.

Akalaza kiti cha gari na kujipumzisa kidogo, na hapo hapo usingizi mzito ukampitia,akalala mazima.

Kwa kawaida watu wanaoamua kulala au kupumzika kando ya barabara au sehemu kama hizo, wanayaacha magari yakiwa yanaunguruma, huku heater ikiwa imewashwa kama ni msimu wa baridi, au AC ikiwa imewashwa endapo ni msimu wa joto.

Ndiyo kusema kwamba lazima gari liwe na mafuta ya kutosha kwa maana ya full tank.

Lakini kwa ndugu yetu kwa sababu ya uchovu ule na kama alivyosimulia yeye mwenyewe baadaye akiwa hospitalini, ni kwamba alipolaza tu kiti kile, usingizi mzito ulimjia na akalala moja kwa moja.

Alisema alichokumbuka yeye ni kwamba gari lake ilikuwa na mafuta nusu tenki tu na gari ilikuwa ikinguruma na alikuwa anajipumzisha tu kidogo ili baadaye aendelee na safari yake.
Cha ajabu usingizi ule ulikuwa wa muda mrefu mpaka alipokuja kustuka baadaye na kuona kwamba miguu yake na sehemu za mbavu tayari zimegandishwa na barafu ambayo ilidondoka usiku ule.

Pia,baadhi ya sehemu za mikono yake nazo zilikuwa zimeanza kuganda,kasoro vidole tu vya mikononi ndivyo vilikuwa vinafanya kazi.

Ndipo kwa taabu aliinua kiwiliwili chake kutoka kwenye kiti cha gari na kuichukua simu yake.

Akapiga simu za dharura, ambapo kikosi cha maafa kilikuja na kumchukua na kumkimbiza kwenda katika Hospitali ya Howard County General,ambako alipelekwa moja kwa moja ICU

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari yake ya kukaa hospitalini hapo kwa matibabu kwa zaidi ya miezi 7 huku akipumulia mashine, akijiuguza mapafu yake ambayo madaktari walisema yalikuwa yamejaa maji.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake mpaka Mungu alipomchukua Septemba 12, 2024.

Nchini Marekani ameacha mtalaka na mtoto wa miaka 14 aitwaye Mpoki.Nchini Tanzania pia aliacha mtoto wa kiume aitwaye Rodgers.
Akiwa hospitalini aliacha ujumbe kwa madaktari kwamba Mpwa wake aitwaye Julius Mwakaleja anayeishi Jimbo la Texas ndiye amsimamie hapo hospitalini wakati wote.

"Julius ukiona nimezidiwa hapa hospitalini wewe ndiye utakayekuja kuzima mashine ya upumuaji ili niondoke zangu," alimwambia mpwa wake huyo na Julius ambaye alimjibu kwamba hilo halitakaa litokee.

"Sitaweza kuzima mashine yako Uncle,nakuahidi, utapona tu,mwamini Mungu," alisema Julius.

Hospitali ilijaribu mara kadhaa kusema apelekwe kituo cha kulelea wagonjwa na kwamba hospitali hapamfai tena,lakini hilo nalo Julius alilipinga sana.

Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba hatimaye amempumzisha mtumwa wake Raymond kwa uamuzi wake Mungu mwenyewe pasipo shinikizo lolote la hospitali wala mtu mwingine yoyote.

Kama ilivyo kawaida ya misiba inayotokea nchini humo,kufuatia msiba huu,jumuiya mbalimbali za Diaspora huko Marekani,zikiongozwa na Julius na marafiki zake zinapambana kichangisha pesa ili mwili wa marehemu uweze kurejeshwa nchini Tanzania.
Lengo likiwa ni kuupumzisha kwenye makaburi ya familia yaliyopo kwenye Kitongoji cha Sumbi,Kijiji cha Usale,Kyela mahali ambapo ndipo alipolala Baba yake Mzee Isaac Anderson Angindike Mwaibila Mwamsiku.



Kwa hapa Tanzania familia ya Asyukile Mwakilima Mwakanyamale wa Kijiji cha Isaki na Thompson Mwakasisi wa Kijiji cha Talatala,Kyela ndizo zinazoratibu msiba huo,wakiongozwa na David Mwakasisi, ambaye marehemu ni mdogo wake kwa Mama mdogo.

Mwili wa Marehemu unatarajiwa kusafirishwa kuletwa nchini Tanzania kuanzia wiki inayoanza Jumatatu Septemba 23,2024.Wale wote wanaomfahamu Raymond pokeeni taarifa za kifo chake.

Rambirambi zinapokelewa na

Kwa walioko nje ya nchi rambirambi itumwe kwa

Julius Thompson Mwakaleja

CashApp: $JuliusMwakaleja

Zelle (913)-271-3767-Julius Mwakaleja

Kwa Tanzania rambirambi itumwe kwa:

Salome Mwakasisi 0755 699 202

Jackson Mwakanyamale 0744841628


Historia ya maisha yake

Raymond alizaliwa Juni mwaka 1969 katika Kitongoji cha Sumbi,Kijiji cha Usale wilayani Kyela, katika familia ya Mama Evelyn Eselina Mwakilima na Mzee Anderson Mwamsiku,ambapo yeye alikuwa ni mtoto wa kwanza.

Elimu ya msingi aliipata katika shule ya msingi Sumbi.Baada ya hapo alisoma shule ya sekondari Ipinda kidato cha kwanza na cha pili, kabla ya kuhamia Sekondari ya Kyela ambayo kwa sasa inaitwa Itope.

Shule zote mbili wakati huo zilikuwa zinamilikiwa na Jumuiya ya Umoja wa Wazazi ya CCM.

Kutoka Kyela sekondari alifaulu vizuri na kuchaguliwa kwenda shule ya serikali ya Kantalamba,Sumbawanga mkoani Rukwa kwa masomo ya HGL.

Hapo Kantalamba alipata elimu ya kidato cha tano na cha sita.Baada ya kupata mafunzo ya JKT alienda kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu na kuhitimu masomo ya Ualimu kikiwemo Kiingrereza na Jiographia.

Baada ya kumaliza masomo hayo alipangiwa kufundisha sekondari ya Kibiti mkoani Pwani ambako alifundisha kwa muda kisha akaona asiendelee ualimu ambao ndio ilikuwa fani yake.

Badala yake akatafuta kazi tofauti na ualimu.Alijikuta anafanya kazi sehemu mbalimbali ikiwemo kampuni ya simu ya Airtel na magazeti ya New Africa na Afrika Leo, ambayo yalikuwa ni magazeti ya kwanza ya mitandaoni nchini Tanzania,na yeye akiwa miongoni mwa Wahariri wake.

Akiwa huko kazini aliomba na kupata nafasi ya kusoma digrii ya upili katika chuo kikuu cha North Virginia ambapo alihitimu Masters Degree in Project Management.

Akiwa nchini humo alishiriki zoezi la kuomba green card,fursa ambayo iko wazi kwa watu mbalimbali duniani kuishi na kufanya kazi nchini Marekani, ambapo alifanikiwa kupata fursa hiyo na ndipo aliamua kubaki nchini humo na kuishi nchini miaka zaidi ya 16 mpaka kifo chake.

Kwa ufupi hayo ndiyo maisha ya Raymond hapa duniani.Mbele yake nasisi zamu yetu inakuja.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa.
Ameen
Imeandikwa na
Benjamin Andongolile Thompson Mwakaleja,
Mpwa wake na Marehemu,
Dar es Salaam,
Tanzania

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news