TARURA yaongeza mtandao wa barabara za wilaya hadi kilomita 144,429.77

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imefanikiwa kuongeza mtandao wa barabara za wilaya kutoka kilomita 108,946.19 hadi kilomita 144,429.77.
Hayo yametangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Na.463 la Juni 25,2021 ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020 hadi 2025.

Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff ameyasema hayo leo Septemba 2,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi cha wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Mhandisi Seff amesema kuwa,mtandao wa barabara hizo umegawanyika katika makundi matatu ikiwemo za lami, changarawe na udongo.

Amesema, hadi kufikia Juni, 2024 barabara za lami za wilaya zilikuwa kilomita 3,337.66 sawa na asilimia 2.31.

Kati ya hizo, Mhandisi Seff amebainisha kuwa, hali ya barabara hizo kilomita 2,743.81 zipo katika hali nzuri, kilomita 445.18 zipo katika hali ya wastani huku kilomita 148.68 zikiwa katika hali mbaya.

Kwa upande wa barabara za changarawe, Mhandisi Victor Seff amesema kuwa, ni jumla ya kilomita 42,059.17 sawa na asilimia 29.12.

Akizungumzia hali ya barabara hizo za changarawe, Mhandisi Seff amesema, kilomita 21,890.53 zipo katika hali nzuri, kilomita 15,792.23 zipo katika hali ya wastani huku kilomita 4,426.41 zikiwa katika hali mbaya.

Vilevile, kwa upande wa barabara za udongo, Mhandisi Victor Seff amesema ni jumla ya kilomita 99,032.93 sawa na asilimia 68.57.

Amesema, kati ya barabara hizo za udongo kilomita 16,118.65 zipo katika hali nzuri, kilomita 34,739.20 zipo katika hali ya wastani huku kilomita 48,175.09 zikiwa katika hali mbaya.

Mhandisi Seff amesema, kutokana na mchanganuo huo barabara nzuri zinaunda jumla ya kilomita 40,752.98 sawa na asilimia 28.22.

Aidha, barabara ambazo zina hali ya wastani ni zaidi ya kilomita 50,926.60 sawa na asilimia 35.26 na zile zenye hali mbaya ni kilomita 52,750.18 sawa na asilimia 36.52.

Mhandisi Seff amesema kuwa, bajeti ya matengenezo ya barabara imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka shilingi bilioni kutoka wastani wa shilingi bilioni 275 miaka minne iliyopita na kufikia shilingi bilioni 850 kuanzia mwaka 2021|2022.

Ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoukabili mtandao wa barabara hizo nchini, Mhandisi Seff amesema, wamejiwekea vipaumbele muhimu vinne ili kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao huo.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo, Mhandisi Seff amesema ni matengenezo ya miundombinu ya barabara ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika nchini.

Pia,kuendelea na matengenezo hata pale barabara na madaraja yanapokamilika ili miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu nchini.

Kipaumbele kingine ni kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za wilaya ili ziweze kupitika katika misimu yote ya mvua.

Mhandisi Seff ameesma, pia wanatumia teknolojia mbadala pamoja na malighafi za ujenzi zinazopatikana maeneo ya kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.

Sambamba na kuzipandisha hadhi barabara kutoka udongo kuwa changarawe,kutoka changarawe au udongo na kuwa barabara za lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii nchini. 

Mhandisi Seff amesema, Serikali imedhamiria kuboresha na kujenga barabara nyingi za wilaya ili kurahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news