TEA na TotalEnergies Marketing Ltd wakabidhi madawati 130 wilayani Kibiti

PWANI-Kampuni ya TotalEnergies Marketing Ltd kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wamekabidhi madawati 130 katika shule ya Msingi Jaribuni Mpakani na Shule ya Msingi ya Kitundu za wilayani Kibiti mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano baina yao katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Hafla ya kukabidhi madawati hayo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti,Kanali Joseph Kolombo katika Shule ya Msingi Jaribuni Mpakani tarehe 24 Septemba 2024.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Kolombo ameahidi kuwa madawati hayo yatatunzwa vizuri kwa manufaa ya wanafunzi wa shule hiyo na kuongeza kuwa Wilaya ya Kibiti imekuwa ikinufaika na miradi kadhaa ya TEA ukiwemo wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Kitundu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd, Bi. Getrude Mpangile amesema madawati hayo 130 ni sehemu ya madawati 200 yenye thamani ya Sh. Milioni 25.9 yaliyotolewa na kampuni hiyo kwa shule tatu za Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.
Kufuatia msaada huyo Shule ya Msingi Jaribuni Mpakani imepata madawati 65, Shule ya Msingi Kitundu madawati 65 na Shule ya Msingi Makuburi ya jijini Dar es Salaam imepata madawati 70.

Bi. Ambangile ameeleza matumaini yake kwamba msaada huo utasaidia kuweka hamasa kwa wanafunzi kujifunza kwa bidii na hivyo kuchangia kukuza ufanisi na ufaulu wa shule zilizonufaika na madawati hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, CPA Mwanahamisi Chambega amekumbusha shule zilizonufaika na msaada huo wa madawati kuyatunza vyema.

“Miongoni mwa majukumu ya TEA ni kutafuta raslimali kutoka kwa wadau mbali mbali na kuzigawa katika taasisi za elimu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia hivyo tunawakumbusha kutunza vifaa hivo,”amesema CPA Chambega.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news