DAR-Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limewapongeza Mwenyekiti wa Bodi, Tido Mhando na wajumbe ndugu Thobias Makoba, ndugu Kingoba Mgaya, Dkt. Rose Reuben, Dkt. Egbert Mkoko na Ladislaus Komanya kwa kuteuliwa kuunda wajumbe wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 19,2024 na Mwenyekiti wa TEF,Deodatus Balile.
"Tunampongeza pia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Slaa aliyefanya uteuzi huu Septemba 18, 2024 na kukamilisha kazi iliyokwamisha utekelezaji wa sheria hii tangu mwaka 2016, yaani miaka minane iliyopita.
"Uteuzi huu ulioanza Septemba 18, 2024 utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
"Ni matumaini yetu kuwa kuteuliwa kwa Bodi ya Ithibati, kutaanzisha mchakato wa kuundwa kwa Baraza Huru la Habari Tanzania (IMCT), ambalo sasa linakwenda kumaliza tatizo sugu la makosa ya kitaaluma kwa wanahabari kupelekwa mahakamani tofauti na taaluma nyingine nchini.
"Tunaamini Mwenyekiti na wajumbe walioteuliwa wataifanya kazi hii kwa weledi mkubwa na kwa masilahi ya kukuza taaluma hasa katika kipindi hiki ambacho vyombo vya habari vina changamoto kubwa ya uchumi.
"Tunawatakia kila la heri na kuwaombea katika kazi hii ambayo taaluma ya habari sasainawekeza matumaini yote kwao.Mungu ibariki taaluma ya habari, Mungu ibariki Tanzania,"amebainisha Balile.