TFRA yawajengea uwezo vijana wanufaika wa BBT kuhusu mnyororo wa thamani wa mbolea

DODOMA-Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo kupitia Vyuo vya Mafunzo vya Wizara ya Kilimo (MATIs) imewajengea uwezo vijana 170 wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika masuala mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Septemba 21 hadi Septemba 22, 2024 kwenye kituo cha BBT Chinangali II jijini Dodoma.

Vijana hao wamepata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na uanzishwaji na uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa mujibu wa Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka 2009.

Akifungua mafunzo hayo,Dkt.Mashaka Mdangi, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka Wizara ya Kilimo amesema kuwa,kilimo ni muhimu kwa mahitaji ya binadamu na viumbe hai kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Mdangi amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kutumia uwezo wao wote kuhakikisha kilimo kinakua ili kiweze kuchangia katika usalama wa chakula na lishe nchini.
Vijana wanaoshiriki programu ya Jenga Kesho iliyobora (BBT) wakijadili jambo wakati wa kikao kazi kilicholenga kuwajengea uwezo ili wazalishe kwa tija.

Pia,kuinua pato la mkulima ili kupunguza umasikini, kuongeza ajira na hatimaye ziada kuuzwa nje na kuwalisha wengine kibiashara kama dira ya Wizara ya Kilimo inavyofafanua.

“Ili tuweze kukuza kilimo hatuna budi kuhakikisha mimea inapata virutubisho na madini stahiki, vitu hivyo vinapatikana kutoka kwenye mbolea.

"Wataalamu watatoa somo hapa na kila mmoja atamaliza mafunzo akiwa ameiva vizuri,” Dkt. Mdangi amesisitiza.

Ameeleza kuwa, fursa iliyotolewa kwa vijana wa BBT na TFRA itakuwa mkombozi kwani mafunzo yanayotolewa yatawasaidia wao pamoja na wakulima wengine watakaosikia shuhuda za kilimo cha kisasa kutoka kwa washiriki wa mafunzo.
“Nimeambiwa kuwa mafunzo haya yanalenga kuwaonesha fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mbolea ambazo ni pamoja na kufanya biashara ya mbolea na kuwa miongoni mwa wauzaji wa mbolea yaani mawakala wa mbolea."

Dkt.Mdangi amesisitiza kuwa, Wizara ya Kilimo inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara ya mbolea ikiwa ni pamoja na uwepo wa takribani ghala 987 zenye uwezo wa kuhifadhi mbolea tani 458,610 nchini.
Dkt. Mdangi amesistiza TFRA na taasisi nyingine chini ya Wizara ya Kilimo zitaendeleza utaratibu wa kufanya mafunzo kama hayo kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vilivyopo nchini.

TFRA imeshauriwa pia kuendelea kuandaa mafunzo kama hayo kwa vijana wengi wanaojihusisha na kilimo ili kutoa uelewa wa masuala ya mbolea.
Meneja wa TFRA Kanda ya Kati, Allan Marik akitoa elimu ya mbolea kwa vijana wa BBT kambini kwao Chinangali II jijini Dodoma leo Septemba 21, 2024.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Kati, Allan Marik amesema, mafunzo yanayotolewa yanajitosheleza katika kumwezesha mshiriki kujihusisha na biashara ya mbolea na kueleza baada ya mafunzo washiriki wote watatunukiwa vyeti vya mafunzo hayo.

Amesema, mafunzo hayo yanalenga kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye miradi ya kimkakati ili kufikia Agenda 10/30; Kilimo ni Biashara yenye lengo la kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakua kwa asilimia kumi ifikapo mwaka 2030.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kufungwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent atakayewatunuku vyeti washiriki 170 wa mafunzo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news