GEITA-Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imekabidhi kadi za bima ya afya 1,093 kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa wakati wa Baraza la Maulid leo Septemba 16, 2024 mkoani Geita.

Katika kukamilisha azma hiyo, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakar Zuber bin Ally na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware walianzisha zoezi la kutoa bima za afya 10,000 kwa watanzania mbalimbali bila kujali tofauti zao.
Awamu ya kwanza ya utoaji bima hizo elfu kumi, Dkt. Saqware amekabidhi kadi za bima 1,093 ambapo kadi 500 ni za kampuni ya Assemble na zilizobaki 593 ni za Kampuni ya Strategis. Mchakato wa kadi zilizosalia 8,907 utaendelea kutekelezwa kwa awamu chini ya kamati maalum ya Mufti ili kufikia ahadi ya kadi elfu kumi.
Bima hizo zimekidhi vigezo vyote vya kisheria na kati ya bima hizo wanaume watapata kadi 448 na wanawake kadi 605. Aidha, kadi hizo zimeshalipia hivyo, wanufaika wataweza kupata huduma za afya na matibabu mwaka mzima bila kugharamia chochote kwenye Hospital zote nchini ambazo zina mkataba na Kampuni au Skimu ya bima ya afya.

Zoezi hili kwa upande wa pili litawaunganisha watanzania wengi bila kubagua wala kujali dini, kabila, jinsia ama umri kwa kua suala la afya ni la wote.