Tumedhamiria kuleta mageuzi makubwa Sekta ya Elimu-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea na mikakati ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa lengo la kuipeleka nchi katika uchumi wa kati na wa juu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Septemba 23,2024 katika kilele cha maadhimisho ya Elimu Bila Malipo kilichofanyika Uwanja wa Amani Complex, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha,Rais Dkt. Mwinyi alifahamisha kuwa ili kufikia lengo hilo, mkazo utawekwa katika kuimarisha sekta ya elimu kwa ajili ya kuwa na wataalamu wengi katika sekta tofauti, na walimu wenye maarifa, ujuzi na weledi.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa miaka sitini ya utekelezaji wa dhana ya Elimu Bila Malipo imefungua milango ya fursa kwa vijana wa Zanzibar kupata maarifa na ujuzi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ndani na nje ya nchi.

Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa walimu kwa kuwapatia mafunzo zaidi, kwani wao ndio nyenzo muhimu katika utekelezaji wa mageuzi hayo.
Rais Dkt. Mwinyi amethibitisha kuwa katika miaka 60 ya Elimu Bila Malipo, nchi imepiga hatua kubwa za maendeleo, kama inavyothibitishwa na ongezeko la ufaulu wa wahitimu katika elimu ya msingi, sekondari, na vyuo vya elimu ya juu.

Vilevile, Dkt. Mwinyi alieleza kuwa Serikali itaendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu katika bajeti yake, ili kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, ujenzi wa maabara za kompyuta, pamoja na ujenzi wa madarasa mpya.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali inakamilisha sera na sheria mpya ya elimu ili kufanikisha mageuzi yanayokusudiwa, pamoja na mchakato wa kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu, itakayokuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi na maslahi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news