ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajipanga kujenga uwanja mkubwa wa michezo utakaokuwa na vigezo vinavyokubalika na Shirikisho la Soka Duniani FIFA pamoja na Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF.
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo Septemba 25, 2024 Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na viongozi na wachezaji wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam waliofika kumsalimia kabla ya mchezo wao wa kesho dhidi ya Azam utakaochezwa Uwanja wa Amani Complex, majira ya saa mbili usiku.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha michuano ya soka inayowashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) na ile ya michuano ya soka ya mataifa ya Afrika kwa timu za taifa (AFCON), kuwa Zanzibar ni sehemu itakayochezwa michezo hiyo.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameelezea dhamira ya Simba ya kujenga kituo cha kuwaendeleza vijana katika mchezo wa soka hapa Zanzibar (soccer academy) kuwa ni jambo jema na kuwaahidi Serikali ipo tayari kuwaunga mkono kwa kuwapa eneo la ujenzi wa kituo hicho.
Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amemuhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kwamba Klabu hiyo ipo tayari kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia utalii wa michezo.