ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameizindua meli ya kwanza ya makontena katika Bandari ya Mkoani na kuwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kuifungua Pemba kiuchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ameshuhudia meli ya Lamu Shipping Limited ikishusha kwa mara ya kwanza makontena kwenye Bandari ya Mkoani, hatua aliyoielezea kuwa ni mapinduzi makubwa kwa sekta ya usafirishaji hapa nchini.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 30 Septemba 2024, alipozungumza na wananchi katika eneo la Bandari Kavu ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Pia, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kinachofanywa na Serikali si kuzikodisha bandari bali ni kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa majukumu ya bandari zote nchini.
Aidha, amefahamisha kuwa, hatua ya kuanza kushushwa kwa makontena kwenye bandari hiyo itarahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji na kuwaondolea wafanyabiashara mzigo wa gharama kubwa.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Pemba kuwa Serikali inaendelea na mipango ya kukamilisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba utakaoanza hivi karibuni, pamoja na ujenzi wa bandari za Shumba, Wete, na Bandari ya Mangapwani, Unguja, ambayo ameielezea kuwa itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli nyingi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa hatua hiyo ya kuifungua Bandari ya Mkoani itaambatana na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa za wafanyabiashara, viwanda vidogo vya kuchakata mwani na mazao ya baharini, pamoja na majokofu. Amehimiza wananchi wa Pemba kuchangamkia fursa hizo.