Tuyaseme hadharani mambo makubwa yanayofanywa na Serikali-Silaa

DAR-Mbunge wa Jimbo la Ukonga ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo, kushirikiana na kuyasema mambo mazuri yote yanayofanywa na Serikali, ikiwepo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani ameweza kuimarisha miundombinu ya barabara, hospitali, shule na huduma nyingi za kijamii hivyo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, ni muhimu wananchi wakachagua viongozi wanaotokana na chama hicho.

Mhe. Silaa ameyasema hayo leo Septemba 09, 2024, katika Mkutano Mkuu wa Kata mbili za Ukonga na Gongo la Mboto, na semina kwa Viongozi wa CCM kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Nimekuja tukumbushane kwamba tunao wajibu wa kuhakikisha tunayasema hadharani mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, hapa Ukonga kuna mambo tulikuwa tunayaona ni ndoto, ametujengea barabara nzuri zikiwepo za mwendo kasi, tuna maji ya uhakika, sasa tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tujipange kuyanadi haya katika uchaguzi huu," amesema Mhe. Silaa.

Awali akimkaribisha Mhe. Silaa kuhutubia katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Ilala na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya Mhe. Juma Mizungu amesema, katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wanachama wa chama hicho wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupiga kura pamoja na kuwachagua viongozi wa CCM.
"Huu ni mwaka wa uchaguzi, zawadi tunayopaswa kumpa mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Kata zote 13 za Jimbo la Ukonga zinaenda kwa CCM, nawaomba sana ndugu zangu, tujitokeze kwa wingi kupiga kura kuchagua viongozi wa chama chetu," amesema Mhe. Mizungu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news