Ulinzi wa maji yanakotoka ni kazi yenu wananchi-Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji wa Mtyangimbole uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Mradi huo ambao unagharimu shilingi bilioni 5.5 unatarajiwa kuvinufaisha vijiji vya Mtyangimbole, Gumbilo, Luhimba na Likalangilo.

Rais Dkt.Samia ameweka jiwe hilo kwa niaba ya miradi 30 leo Septemba 24,2024 akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Ruvuma huku akiwataka wananchi kutunza chanzo cha maji hayo.
"Ninashukuru sana kwa kufika eneo hili la Mtyangimbole kwa kazi ya kuweka jiwe la msingi kwa miradi 30 inayoendelea ndani ya mkoa huu.

"Mradi huu, unakwenda kuhudumia vijiji vitatu ndiyo makusudio, lakini maji yatabaki yatakwenda kwenye kijiji kingine cha nne.

"Ndugu zangu mnakumbuka wakati wa kipindi cha kampeni tuliahidi kumtua mama ndoo kichwani. Sasa tumekwenda kufanyia kazi ahadi ile, tumeifanyia kazi kwa kusambaza maji nchi nzima.

"Kama mnavyoona tulivyofanya Ruvuma na nchi nzima ni hivyo hivyo, kwa hiyo tunatarajia ikifika mwaka kesho 2025 tuwe tumetimiza lile lengo ambalo tumetumwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba vijiji vyote vya Tanzania vipate maji kwa asilimia 85.
"Tutakuwa tumelitimiza au tutakuwa tumelipita kidogo,lakini na kwa mijini ni hivyo hivyo, kwa mijini tumetumwa tupeleke maji kwa asilimia 95 na tayari baadhi ya miji inapata maji kwa ukamilifu ukiwemo Mji wa Songea utapata maji kwa asilimia 100.

"Kwa hiyo tunatarajia hata kile kipimo tulichopewa na Ilani ya CCM tutakuwa tumepita. Nilikuwa ninaangalia mfumo wa mradi huu, chanzo kikubwa ni mto.

"Chanzo kile kinatoa maji mengi, ndiyo maana nimesema yatabaki mengine n vijiji vingine vitapata, ombi langu kwenu ni kutokuharibu kile chanzo cha maji. Ule ndiyo uhai wenu, maji haya yatatumika kwa matumizi ya binadamu, wanyama lakini pia kwenye kilimo kwenye baadhi ya maeneo.

"Kwa hiyo, niwaombe sana sana...sana msiende kuharibu kile chanzo ambacho kinatupa uhai huu, kule mtoni twende tukatumie, lakini kuwe na ulinzi wa kutosha.
"Walinzi wa mwanzo wa chanzo kile muwe wenyewe wananchi na siyo watu wa maji, watu wa maji kazi yao kuangalia maji yako wapi, watafanya nini maji yasambae yawafikie wananchi.

"Lakini, ulinzi wa maji yanakotoka ni kazi yenu, kwa hiyo niwaombe sana sana muendelee mkailinde rasilimali yenu ambayo itawaletea uhai katika maisha yenu,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameahidi changamoto ndogo ndogo ambazo viongozi wao wamezielezea, Serikali itazipatia ufumbuzi kama walivyofanyia kazi mambo mengine.

"Ili mradi wananchi wetu wapate kukaa kwa raha, maji wapate, chakula kipatikane na mimi niwashukuru watu wa Ruvuma ni wakulima wakubwa sana, mnalima hadi tunapata ziada ya kuuza nchi jirani.
"Lakini, elimu ipatikane na afya mambo yaende vizuri, tunajitahidi katika maeneo hayo yote kufanyia kazi ili wananchi wapate huduma stahiki wanazozihitaji,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.
Rais Dkt.Samia ameweka jiwe la msingi mradi huo wa tenki la maji Mtyangimbole ambao una uwezo wa kupokea lita milioni 1.9 na utahudumia wananchi zaidi 14,000.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news