Upandikizaji mimba, ukombozi familia

NA LWAGA MWAMBANDE

SEPTEMBA 12,2024 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Philip Mpango amehimiza uwekezaji uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wa upandikizaji mimba pamoja na uwashaji wa vifaa vya kusaidia kusikia kwa watu wenye changamoto ya kusikia kuwa endelevu.
Dkt.Mpango ametoa wito huo wakati wa hafla ya kuzindua Kituo cha Upandikizaji wa Mimba, kuwasha Vifaa vya Kusaidia Kusikia kwa Watoto na Kuzindua Gari la Huduma Tembezi za Afya (Mobile Medical Service) iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Amesema,ni muhimu kuondokana na utegemezi wa wataalam kutoka nje na lazima jitihada za makusudi zichukuliwe ili kuwezesha uhamishaji wa teknolojia na ubunifu.

Makamu wa Rais Dkt.Mpango ameiagiza Wizara ya Afya kuandaa mpango madhubuti wa kuwajengea uwezo wataalam wa ndani watakaoweza kuvitumia na kuvifanyia ukarabati vifaa vyote vya kisasa, pindi hitaji hilo litakapojitokeza.

‘’Uzinduzi wa huduma za upandikizaji mimba na vifaa vya usikivu ni hatua muhimu sana katika kusaidia wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uzazi na watoto waliozaliwa wakiwa na changamoto ya usikivu.

‘’Ni faraja kuona huduma ya upandikizaji wa mimba inaanza kutolewa kwa mara ya kwanza nchini katika Hospitali ya Umma,”amesema Dkt.Mpango.

Kutokana na mafanikio hayo ya kihistoria katika Sekta ya Afya nchini, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema ni jambo jema na lenye tija kubwa kwa familia. Endelea;

1. Upandikizaji mimba, hili jambo kwetu jema,
Lawagusa wengi wamba, ambao walishakwama,
Walizihesabu namba, kusaka mwana kwa ngama,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

2. Sipitali Muhimbili, maendeleo ni mema,
Utasa waenda mbali, na shida za kinamama,
Wanafika kwa kivuli, mbele hakuna kukwama,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia

3. Kuna baadhi ya ndoa, walio baba na Mama,
Ziliyumba zilipoa, pa mwana kusimama,
Sasa mbegu wakitoa, mimba yabebwa salama,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

4. Yaliyofanyika nje, hapa wengi walikwama,
Gharama zile za nje, jinsi zilivyosimama,
Sasa angalau punje, Serikali yetu njema,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

5. Maisha yaendelee, kwa kinababa na Mama,
Neema muipokee, muitwe baba na Mama,
Hili jambo la pekee na tena lililo jema,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

6. Mliokata tamaa, ile ya kuitwa Mama,
Acheni kukaakaa, hii habari ni njema,
Ujasiri wenu vaa, mimba ziweze simama,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

7. Tena tekinolojia, kwa jinsi ilivyo njema,
Wamama wazima pia, hawawezi wakakwama,
Mara watafurahia, mimba zinavyosimama,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

8. Pongezi kwa Serikali, kulifanya hili jema,
Kweli imeona mbali, hasa kwa akina Mama,
Vile wasemwa vikali, vipi mimba zinakwama,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

9. Huku ni kujali watu, ambako tunakusema,
Sisi wenyewe ndo watu, shida za mimba zakoma,
Sasa ni matumizi tu, waongezeke wamama,
Upandikizaji mimba, ukombozi familia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news