DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema sekta ya uvuvi inaingiza mapato ya sh. trilioni 2.94 kwa mwaka na imekuwa ikikua kwa wastani wa asilimia 1.9 kwa mwaka.

Ameyasema hayo leo Jumatano, Septemba 11, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) wanaohusika na masuala ya Uvuvi, Bahari, Maziwa na Mito ulioanza leo kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema kila siku watu 230,000 wanajishughulisha na uvuvi mdogo na Watanzania takriban milioni sita wamepata ajira zisizo za moja kwa moja kwenye sekta hiyo.
“Uvuvi mdogo mdogo unachangia zaidi ya asilimia 95 ya mavuno yote ya samaki nchini,”amesema.
Akielezea fursa za uwekezaji kwenye ufugaji wa samaki, amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuendeleza sekta hiyo kutokana na rasilimali kubwa za maji ilizonazo ikiwa ni pamoja na Bahari ya Hindi, maziwa, mito, mabwawa mengi ya asili na yaliyojengwa na binadamu.

"Hivi sasa, uvuvi wa kibiashara katika eneo hilo unafanywa hasa na Mataifa ya Uvuvi wa Maji ya Mbali (Distant Water Fishing Nations) chini ya mikataba ya leseni za uvuvi.”
“Eneo Maalum la Kiuchumi la Tanzania ni fursa kubwa ya uwekezaji kupitia ununuzi wa meli za uvuvi, uwekezaji wa huduma za meli, usambazaji wa vifaa vya uvuvi, usambazaji wa chakula (maji, chakula na matunda), kuongeza thamani na usindikaji, utafiti na ulinzi wa baharini na angani.”
Amezitaja fursa nyingine za uwekezaji kuwa ni pamoja na uvuvi wa kina kirefu kwa ajili ya samaki aina ya tuna; kilimo cha mwani; uzalishaji wa vifaranga na chakula cha samaki.
“Aidha, kuna fursa kubwa katika eneo la usindikaji wa samaki na miundombinu ya hifadhi ya bahari,” ameongeza.