Viongozi mabubu wamchefua Rais Dkt.Samia

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameonesha kusikitishwa na tabia za baadhi ya viongozi walioaminiwa katika nafasi mbalimbali, ambao wamekuwa na tabia ya kukaa kimya bila kutoa ufafanuzi pale wenye nia ovu wanapozusha mambo na kuwaaminisha wananchi kuwa ni ukweli.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyabainisha hayo Septemba 26,2024 wilayani Tunduru ikiwa siku za karibuni yameibuka baadhi ya makundi ya watu wenye nia ovu kuamua kutengeneza mambo ambayo hayana ukweli huku wakiamua kupotosha mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ikiwemo miradi ya maendeleo.

“Suala la kuchanganya picha za kuzusha zinazorushwa katika mitandao, ndugu zangu Watanzania kama kunarushwa picha ya uongo katika mitandao, katika maeneo yetu kuna wakuu mbalimbali wapo.
"Lakini hakuna anayekanusha kwamba hiyo picha sio ya leo, kwamba hiyo hospitali au hilo eneo sasa hivi liko kwenye hali hii na ikapigwa picha ikaingizwa kuondoa ule upotovu uliofanywa, sijui tunaelekea wapi?.

“Kwamba mpaka aje Rais na mawaziri wasimame wakanushe wakati mnaozuliwa hiyo hali mpo, hii sio sawa.

"Hii ni sawa mwanaume kaingia nyoka ndani ya nyumba yako unatoka mbio unaenda kumuita mwanaume mwenzio njoo unitolee nyoka nyumbani kwangu, ujana dume uko wapi hapo?.
“Kama kwenye nyumba yako unazushiwa, maendeleo yanakuja, Serikali inashughulika, fedha zinatoka, mambo yanafanywa,lakini anatoka mpuuzi mmoja anaweka picha za ajabu ajabu na wote mmenyamaza kimya.

"Hi sio sawa mnatutia wasiwasi ndugu zangu, viongozi mna shida gani? Mnafanya nini? Mnatutia wasiwasi, unapoona kidole kinakuja jichoni kwako jilinde lisitoboke.
"Sasa hivi kipindi tulicho hiki yatakuja mengi, sasa mkishindwa kukanusha tutajua hatuna viongozi upande huu,”amesisitiza Rais Dkt.Samia wakati akizungumza na wananchi katika Uwanja wa CCM wilayani Tunduru ikiwa ni siku ya nne ya ziara yake mkoani Ruvuma.

Waziri

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema,hakuna mgonjwa anayesafirishwa kwa njia ya pikipiki huku akiwa amewekwa kwenye tenga kupelekwa kupata huduma za afya.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati akitoa salaam za wizara kwenye mkutano huo wa hadhara wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Nimeona taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha mgonjwa akisafirishwa kwenye pikipiki huku akiwa kwenye tenga na kueleza kuwa hakuna magari ya kusafirishia wagonjwa na kwa yaliyopo huwagharimu wananchi fedha nyingi kwa ajili ya kupata huduma ya gari la wagonjwa.

"Napenda kukuthibitishia Mheshimiwa Rais hapa Tunduru hakuna upungufu wa magari ya kubebea wagonjwa na kati ya magari 535 tuliyoyakabidhi mwaka jana kwa muongozo wako Mhe. Rais hapa Tunduru walipata magari manne ya kubebea wagonjwa.
"Na magari hayo yalipekwa kwenye Kituo cha Afya Nakapanya, Matemanga, Mtesi na Kituo cha Afya Nyalasi ambayo yanafanya kazi saa 24 na rufaa zote zinaratibiwa kwa utaratibu maalumu na sio kuchangisha wananchi.

"Utaratibu unaotumika kusafirisha wagonjwa nikutumia magari ya kubebea wagonjwa (Ambulaces) na kwa kutumia madereva ngazi ya jamii waliosajiliwa wakati wa mfumo wa M-Mama ambapo mfumo huu unahusika na kusafirisha akina mama wajawazito na watoto wachanga bila malipo yoyote."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news