RUVUMA-Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imewahukumu Mwenyekiti wa Majimaji AMCOS Tunduru, Issa Rashid Makopi,Meneja Msaidizi Majimaji AMCOS Tunduru,Mtuva Saidi Rashidi,
Meneja Majimaji AMCOS Tunduru, Mfaume Zuberi Mambo na Meneja Naluwale AMCOS Tunduru,Halifa Saidi Chipangula adhabu ya kulipa faini ya shilingi milioni 1.5 na kifungo cha miaka miwili jela.
Washtakiwa hao walishtakiwa kwa kutoa hongo sh. 800,000 kwa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU0 Wilaya ya Tunduru,Geoge Alanus Njogolo ili asiendelee na uchunguzi dhidi yao uliohusu ubadhirifu wa mbolea aina ya salfa inayotolewa bure na Chama Kikuu cha Ushirika (W) Tunduru (TAMCU LTD).
Mbolea hiyo hutolewa kwa wakulima wa korosho waliopaswa kupewa na viongozi hao na makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 15 (1) (b) na(2) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [Sura ya 329 mapitio ya 2022].
Hukumu dhidi ya Viongozi wa Majimaji AMCOS Wilaya Tunduru katika shauri la jinai Na. 26462/2024 ilitolewa Septemba 18, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya Tunduru Bw. Shughuli J Mwampashe (SRM), akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Mwinyi Yahaya.
Washitakiwa wametiwa hatiani na Mahakama imewahukumu kulipa faini ya Shilingi 1,500,000 na kutumikia kifungo cha miaka 2 jela.
Pia fedha sh. 800,000 imetaifishwa na kuwa mali ya Serikali na imeamriwa iwekwe katika akaunti ya Kamanda Uchunguzi Ruvuma.
Washitakiwa wamelipa faini jumla ya Shilingi 1,500,000 na sasa wanatumikia kifungo cha miaka 2 jela.
Tags
Habari
Mahakamani Leo
Rushwa ni Adui wa Haki
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)