Waambieni mimi ni muuaji wa mambo haya, lakini sijawahi kuua mtu labda sisimizi-Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wa chama hicho ikiwemo Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) kujibu hoja zinazoibuliwa kwa ajili ya kumshambulia yeye na Serikali.
Dkt.Samia ameyasema hayo leo Septemba 28,2024 wakati akifunga Kikao Maalum cha Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Taifa.

Ni katika ukumbi wa Parokia ya Bombambili katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

"Nimesikia hapa kwa masikitiko makubwa mnazungumzia yanayosemwa kwa mwenyekiti wenu, anavyosemwa, anavyoshambuliwa, anavyoambiwa. Sasa, ombi langu kwenu ni kusimama imara.

"Ukweli mnaujua, ukweli mnaujua...mdomo wa mwenyekiti mmoja kujibu hoja zile hautoshelezi.Na pengine mwenyekiti wakati hayo mambo yanatokea niko kwenye majukumu mengine na mambo mengine.

"Msimame na mjibu ndugu zangu, mnahofia nini? Msimame tu mjibu, hakuna cha kuhofia hapa, mkiambiwa mwenyekiti wenu, Rais wenu muuaji, waambieni ni kweli ameua nguvu hasi ya upinzani.

"Mkiambiwa mwenyekiti wenu, Rais wenu muuaji waambie kweli ameua njia zote za kuzidisha umasikini ndani ya nchi hii na amekuza uchumi wa nchi hii.

"Kwa hiyo, tumeua yale mambo hasi ya kuturudisha nyuma kiuchumi, na tumekuza uchumi. Mkiambiwa mwenyekiti na Rais wenu ni muuaji, waambieni ni kweli ameua giza lililofunika Tanzania, na kwamba sasa Tanzania, katika kiwango cha Kimataifa inang'ara.

"Hayo ndiyo niliyoua Rais wenu na mwenyekiti wenu, sijawahi kuua mtu, labda sisimizi nimeua, lakini siyo mtu. Kwa hiyo, ndugu zangu simameni tu mjibu,simameni tu mjibu.

"Mkiona tu, hivyo nataka niwaambie sisi wote ni wazazi hapa, toto lako likija limeshakuudhi hasa wa kiume unataka kumtandika anatoka mbio, akitoka mbio haumpati ameshakushinda...unabakia nini...litizame....huna adabu....ndiyo yanayotokea ndugu zangu.

"Ndiyo yanayotokea, hawa watu hawana pa kushika, kwa hiyo sasa lililobakia muoneni yule mwana..kadha wa kadhaa,sasa ndugu zangu jibuni tu,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news