DODOMA-Wadau wa Sekta ya Ununuzi wameaswa kutumia vyema mifumo ya ununuzi kwa njia ya kieletroniki hususan Moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa inayopatikana katika mfumo wa NeST.

Bw. Kiwango amesema kuwa anaamini kupitia kikao kazi hicho washiriki sasa hawatarudi tena nyuma, bali wataendelea kutumia moduli hiyo kuwasilisha malalamiko na rufaa kwani huokoa muda na gharama.
“Nawiwa kuamini ya kwamba katika kutekeleza zoezi la kuipitia moduli, mbali na kutoa maoni ya maboresho yanayopaswa kufanyika, mmeweza kujifunza namna moduli hii inavyofanya kazi, hususan kwa kuyaelewa vyema majukumu yenu ninyi kama taasisi nunuzi ambao ni wadau wakubwa katika matumizi ya moduli,” alisema Bw. Kiwango.
Pamoja na mambo mengine, amewapongeza wataalamu kutoka Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) na Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kuandaa moduli hiyo ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa Umma kwa njia ya kielektroniki.
“Hii ni hatua kubwa katika historia ya ununuzi wa umma nchini, hususani katika kuhakikisha kuwa mchakato wa zabuni na malalamiko yanayotokana na michakato hiyo vyote vinafanyika kielektroniki, hongereni sana wataalamu,” alisema Bw. Kiwango.
