Wadau wa utalii watoa neno miundombinu ya barabara Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

SERENGETI-Wadau wa utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wameipongeza Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa jitihada zinazoendelea kufanyika ili kuhakikisha wanarejesha barabara zilizoharibika wakati wa msimu wa mvua.
Pia,wameiomba Serikali kuja na suluhisho la kudumu la ujenzi wa barabara katika Hifadhi za Taifa hususani Barabara ya Serengeti ambayo inahudumia magari zaidi ya 600 kwa siku.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha ametoa pongezi hizo leo wakati akizungumza na wanahabari.
Amesema,maboresho ya barabara hizo ambazo kwa kiasi kikubwa ziliathiriwa na mvua zilizonyeesha mwanzoni mwaka huu yanaleta matumaini kwa wadau.

Macha pia ameyasema hayo mbele ya Kamishna ya Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Nassoro Juma Kuji, ambaye alifanya ziara ya kukagua matengenezo yanayoendelea kufanyika katika barabara ya Naabi hadi Seronera.

Kutokana na hali hiyo, wadau hao wamependekeza kujengwa kwa barabara yenye tabaka gumu katika hifadhi hiyo ikiwa ni mwarobaini wa tatizo la barabara.
“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo.

"Lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili.

“Kwa hiyo lile wazo Serikali kupitia Serengeti la kuwa na tabaka gumu la kudumu lingekuwa wazo zuri sana wakati huu tungesahau matengenezo haya ya mara kwa mara na hata kuongeza gharama ni bora tuingie gharama kutengeneza barabara itakayokaa muda mrefu hata kama ni gharama kubwa,” amesema Macha.
Januari 26, 2024 Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Nassoro Juma Kuji alifanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza menejimenti ya hifadhi hiyo, kushughulikia kwa haraka maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi ili watalii wafikie azma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Kutokana na hali hiyo aliilekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika licha ya uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ili kupunguza adha kwa wageni.
“Licha ya changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea hatuwezi kusubiri ziishe tumeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka.

"Lakkini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” alisema Kamishna Kuji.

Aidha, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchi nzima.

Pamoja na hali hiyo, Kamishna Kuji amebainisha kuwa TANAPA inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi za Taifa nchini inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea hifadhi hizo zilizosheheni sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mvua kubwa zilizonyesha tofauti na miaka mingine.

“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” alisema.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Stephen Msumi alisema kuwa, menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali.

Ni katika hifadhi ikiwemo kudhibiti mwendokasi alama mbalimbali za barababra ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
Hifadhi ya Taifa Serengeti hivi karibuni imekumbwa na changamoto ya barabara kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Nchini na kuharibu miundombinu ya barabara hizo

Ukarabati unaofanywa na TANAPA utaondoa adha hiyo na kuzifanya barabara zote ndani Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news