BANGALORE-Ujumbe kutoka Tanzania umefanya ziara ya mafunzo huko jijini Bangalore, nchini India kuanzia Septemba 15 hadi Septemba 20,2024.
Ziara hii iliyoandaliwa na kudhaminiwa na Mfuko wa Bill & Melinda Gates ililenga kubadilishana ujuzi na uzoefu juu ya Utumiaji wa Mfumo wa Wazi wa Vitambulisho vya Kidijitali (Modular Open Source Identity Platform (MOSIP) and Digital Public Infrastructure (DPI)) katika kuongeza wigo wa huduma jumuishi za fedha nchini.
Ujumbe huu ulijumuisha wadau kutoka Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Wadau wengine ni Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA); Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA), Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Tanzania Bara (RITA), Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Tume ya Mipango na Financial Sector Deepening Trust (FSDT).
Ujumbe wa Benki Kuu ya Tanzania, ambayo ni Sekretarieti ya Taifa ya Kamati ya Huduma Jumuishi za Fedha, uliongozwa na Naibu Gavana (Usimamizi na Uthabiti wa Sekta ya Fedha), Bi Sauda Msemo.
Moja kati ya mipango ya Mkakati wa Tatu wa Huduma Jumuishi za Fedha Tanzania (Tanzania National Financial Inclusion Framework III) katika kufanikisha lengo kuu la upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha nchini, ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uwezo kupata huduma mbalimbali za fedha popote alipo.
Kwa sasa, lengo hili linaathiriwa na kukosekana kwa vitambulisho vya kidijitali kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18.