Wakulima Mbinga wamkosha Rais Dkt.Samia, awashauri

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan amepongeza juhudi za wakulima katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kufanya nchi kuwa na usalama wa chakula.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa pongezi hizo leo Septemba 25,2024 katika muendelezo wa ziara yake ya siku sita mkoani Ruvuma wakati akiwasalimia wananchi katika Kituo cha Ununuzi wa Nafaka cha Mbinga Sokoni.

Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amewataka wakulima kujiepusha na walanguzi huku akiwataka kuuza mahindi kwa bei elekezi ya Serikali ya shilingi 500 hadi 600 kwa kilo au katika Kituo cha Wakala wa Taifa wa Chakula (NFRA) kwa shilingi 700.

Mbali na hayo, Rais Dkt.Samia amewataka wakulima kuhakikisha wanapanua mashamba yao na kuepuka kutumia vibaya mapato wanayoyapata.

Amewaeleza kuwa,kahawa wanauza bei nzuri, hivyo wasichezee fedha. "Niwaombe sana pesa zile tusichezee, ngoma zikaisha,pesa tuweke akiba kwa mambo ya baadaye, tutanue mashamba zaidi.

"Leo tunatoa ruzuku, lakini huko mbele pengine tutasema sasa wakulima jitegemeeni. Serikali katika kuwaonea huruma imeleta mtandao wa ununuzi wa mahindi, ninaomba kauzeni kwenye mtandao wa Serikali, msije mkatoa mahindi mkaumizwa, mtakuwa mnajiumiza wenyewe.

"Ukienda kuuza serikalini NFRA unapewa shilingi 700 kwa kilo, wakati walanguzi wanawapa shilingi 300 kwa kilo, hiyo ni kujidhulumu wenyewe."

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussen Bashe amewahakikishia wakulima kuwa, Serikali inaendelea kutoa ruzuku na mbolea ikiwemo mbegu.

Vilevile, amepongeza uzalishaji wa kahawa aina ya Arabika ambapo wakulima wa Mbinga wamrepata mauzo bora ya dola milioni 5.6 ikilinganishwa na wastani wa Kitaifa wa dola milioni 4.7.

Aidha, Serikali imesema imeanza kushughulikia changamoto za ushirika na mfumo wa kangomba ili kuhakikisha wakulima wanalipwa ndani ya siku 48.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news